Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wapili kulia) akifuatiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella  na kulia ni Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Fredy Mahobe wakimsikiliza  Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico Dkt Venance Mwasse akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi wa kiwanda cha kuchakata dhahabu kinachojengwa mkoani Mwanza
 Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa kwanza kulia) na wajumbe alioambatana nao wakimsikiliza  Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico Dkt Venance Mwasse akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi wa kiwanda cha kuchakata dhahabu kinachojengwa mkoani Mwanza
 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico Dkt Venance Mwasse akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi wa kiwanda cha kuchakata dhahabu kinachojengwa mkoani Mwanza mbele ya Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na wajumbe alioambatana nao katika ziara ya kikazi mkoani Mwanza leo tarehe 12/05/2020.

 Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na ujumbe ulioambatana naye wakiendelea na ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata dhahabu mkoani Mwanza

 Mshauri Mwelekezi na Msimamizi wa ujenzi wa kiwanda cha kuchakata dhahabu kinachojengwa mkoani Mwanza Libaan Yasir akionesha katika ramani namna jengo la kiwanda cha kuchakata dhahabu kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella  na wajumbe walioambatana nao katika ziara hiyo.
 Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akifuatana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella wakihitimisha ziara ya kukagua jengo la kiwanda cha kuchakata madini ya dhahabu mkoani 
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo kushoto akiagana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico Dkt Venance Mwasse mara baada ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho kuhitimishwa

Stamico ,Mkandarasi wamkosha Naibu Waziri Nyongo 

Mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kuchakata madini ya dhahabu nchini umeshika kasi huku ujenzi wake ukitarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Septemba 2020 na kuifanya dhahabu ya Tanzania kusafirishwa ikiwa tayari imechakatwa na hivyo kuongeza thamani ya madini hayo katika soko la dunia.

Ujenzi wa kiwanda hicho ulianza rasmi mwezi Machi 2020 ambapo ujenzi wake mpaka sasa umefikia asilimia 40, imeelezwa kuwa kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda hicho utapelekea suala la kisheria la kutokusafirisha madini ghafi kutekelezwa ipasavyo.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 12 Mei, 2020 wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo baada ya kutembelea eneo la ujenzi wa kiwanda hicho na taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho unaoendelea kwa kasi Mkoani Mwanza kutolewa.

Akizungumzia mabadiliko ya sheria ya madini ya mwaka 2017, Naibu Waziri Nyongo alisema kukamilika kwa kiwanda hicho kutakwenda sanjari na sheria inayowataka wafanyabiashara   wa madini kutokusafirisha madini ghafi na badala yake madini yote kusafirishwa yakiwa yamechakatwa na kuongezewa thamani itakayopelekea kuuzwa kwa bei nzuri katika soko la dunia.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika eneo hilo la ujenzi, Naibu Waziri Nyongo alikiri kufurahishwa na usimamizi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na kasi ya mkandarasi anayesimamia ujenzi wa kiwanda hicho na kukiri kuwa Serikali itakuwa ikitembelea eneo hilo mara kwa mara katika  ili kuhakikisha ujenzi wake unakamilika kwa wakati na kiwanda kufunguliwa kwa wakati kama inavyotarajiwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse ameeleza kuwa ukamilishwaji wa mradi huo utakwenda sambamba na mradi wa kuwawezesha wachimbaji wadogo katika suala zima la kusafisha dhahabu waliyochimba katika maeneo yao.

Aidha, Dkt. Mwasse amesema msaada utakaotolewa kwa wachimbaji wadogo kutasaidia kiwanda hicho kupata malighafi zakutosha kwa ajili ya kulisha kiwanda kinachotarajiwa  kuzalisha kg 480 za dhahabu kwa siku yenye purity ya kiasi cha 999.99 ambacho ni kiwango cha juu kabisa cha purity ya dhahabu duniani.

Akielezea usafi wa dhahabu itakayokuwa ikizalishwa katika kiwanda hicho, Dkt. Mwasse amesema dhahabu hiyo itakuwa na thamani ya fedha kwa viwango vyake na hivyo yaweza kuhifadhiwa katika Benki Kuu ya Tanzania kama akiba.

Aidha, Dkt. Mwase amesema yeye na Taasisi anayoisimamia, wanajisikia fahari kubwa kusimamia azma ya serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda na wao wakiwa ni miongoni mwa taasisi inayosimamia viwanda mahususi kwa ajili ya kuongeza thamani ya madini nchini na kukiri shirika la madini linatekeleza azma hiyo kwa vitendo.

Pamoja na hayo, Dkt. Mwasse ameahidi kusimamia kikamilifu suala la utoaji wa kodi ya huduma pamoja na Uwajibikaji wa kiwanda hicho kwa jamii inayozunguka mradi huo katika kutatua masuala mbalimbali ya kijamii kama sheria inavyoelekeza.

Kwa upande wake, Mkandarasi wa ujenzi wa kiwanda hicho Libaan Yasir wa kampuni ya Aqe Associates LTD alikiri kuwa mradi huo ulipangwa kukamilika mwezi Desemba mwaka 2020 lakini kwa namna alivyojipanga pamoja na timu yake watakamilisha ujenzi wa kiwanda hicho ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: