Spika wa Bunge, Job Ndugai amemtaka Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kurejesha Tsh milioni mbili alizopewa na Bunge ili kuhudhuria vikao vya Bunge lakini hakuhudhuria na kutimkia karantini pamoja na baadhi ya wabunge wake wa chama hicho.

Ndugai amesema hayo leo Mei 18, 2020, Jijini Dodoma na kusisitiza kuwa, lazima Mbowe arejeshe fedha hizo na kumtaka asiwapelekeshe wabunge wake .

Ameongeza kuwa wabunge wa chama chake wakipata mishahara wanakatwa pesa zao
“Kwanza kama mbunge wangu namshauri, kuzungumza baada ya kiongozi wa nchi kuzungumza na taifa na kuanza kuzodoa kile ambacho amekizungumza ni kujipima ubavu na mkuu wa nchi. Namshauri Mbowe afanye kazi na Rais, ukimdharau Rais maana yake umetudharau sisi sote, namsihi ajiepushe asiende njia anayokwenda.

“Hata mwandishi ukichukua fedha ya kazi halafu usiende kwa kusema umejiweka lockdown watakushangaa, kuna Wabunge wengine wamerudisha fedha, wengine bado akiwemo Mbowe niombe arudishe, na hiyo fedha lazima itarudi tu, njia gani nitaitumia niachieni mimi.

“Walio wengi wamerudisha lakini wengine bado akiwemo yeye Mheshimiwa Mbowe na ndo ubaya wangu unapokuwa hapo nichukue nafasi hii kumwambia milioni mbili na elfu 40 lazima arudishe ni taratibu za kifedha, mimi kusimamia taratibu za kifedha ni wajibu wangu.

"Atumie nafasi yake ya kiongozi wa upinzani bungeni kushauri na siyo kuropoka, sehemu yake sahihi ni bungeni na siyo sehemu nyingine. Mbowe kama kiongozi wa upinzani bungeni anapewa ofisi, secretary, mhudumu, dereva, gari, nyumba, marupurupu, posho, senior officer, Sasa anachotaka kingine ni nini? Yaani yeye kila kitu anapinga, hiyo siyo sawa, namsihi aache.

“Mpaka leo tarehe 18 tunavyoongea Freeman Mbowe hajarudisha fedha ni kuonesha kwamba alikuwa na nia ovu, nina hakika hizo fedha zitarudi msiwe na wasiwasi, ni njia gani nitatumia msiwe na wasiwasi, hapo ataniona mbaya, wenzake wengi wao wamekwisharudisha.

“Mheshimiwa Mbowe tumeingia wote mwaka 2000 Bungeni, miaka 5 ya Mkapa Mbowe na wenzake walipiga kura za hapana katika mambo yote, kipindi cha Kikwete miaka 5 walisema hapana kwa mambo yote, kipindi cha Magufuli wao walitoka nje. Nisikitike kusema ndugu yetu huyu ni mtoro sana na ninyi waandishi ni mashahidi hatumsingizii, anapenda kufanya vitu nje ya Box, anapitwa na mambo mengi, akitoka nje anamshutumu Spika."- Amesema

Aidha, Spika wa Bunge Job Ndugai amesema Rais Magufuli atahitimisha Bunge Juni 16,2020 jijini Dodoma badala ya Mei 29,2020 iliyopangwa awali ili kufuata kalenda ya usomaji bajeti ya Jumuia ya Africa Mashariki.
Share To:

Post A Comment: