Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof.Shadrack Mwakalila amewataka watumishi wa Chuo hicho  kutekeleza majukumu yao ya kazi huku wakizingatia maelekezo yanayotolewa na Serikali ya namna ya kujikinga dhidi ya  virusi vya ugonjwa wa korona (COVID 19).

Prof. Mwakalila ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa Kampasi ya Karume- Zanzibar na kusisitiza kuwa kufuatia
maelekezo ya Serikali ya kufungua vyuo nchini, Chuo hicho kimejiwekea mikakati mbalimbali ya kukabiliana na ugonjwa wa korona wakati wa utekelezaji wa majukumu yake makuu ambayo ni kufundisha, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa jamii inayokizunguka.

“Pamoja na mambo mengine Chuo kimejiwekea mikakati mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa wanafunzi na watumishi juu ya ugonjwa wa korona, kutumia ubunifu na TEHAMA katika kufundisha na kuhakikisha maelekezo ya kuwepo kwa Maji tiririka, vitakasa mikono, matumizi ya barakoa, na kuwepo kwa umbali wa mtu mmoja na mwingine,”alisisitiza Prof. Mwakalila.

Akizungumza na watumishi hao Naibu Mkuu wa Chuo anaesimamia Mipango, Fedha na Utawala Dkt.Godwin Kaganda amewataka   viongozi na watumishi wote kuhakikisha wanazingatia kwa makini matumizi ya vitakasa mikono na kuhakikisha vinapatikana muda wote na kusisitiza kuwa viongozi wafanye kazi kwa ushirikiano ili kufikia malengo.


Naye Mkuu wa Kampasi ya Karume- Zanzibar Dkt.Rose Mbwete amewataka watumishi kuhakikisha wanafanya kazi kwa kufuata miongozo,kanuni, taratibu na sera za chuo ili kufikia malengo.


IMETOLEWA NA KITENGO CHA UHUSIANO
CHUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE
KAMPASI YA KARUME-ZANZIBAR.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: