Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali kupitia Chadema, amemwaga chozi ndani ya ukumbi wa Bunge jijini Dodoma wakati akitangaza kujiondoa Chadema pindi Bunge litakapomaliza muda wake huku akieleza namna alivyokipigania chama chake, lakini kwa sasa hawamthamini.

Lijualikali amesema hayo Bungeni leo Jumatatu, Mei 18, 2020 na kumtuhumu Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwa unyanyasaji kwa wabunge na matumizi yasiyo halali ya fedha ikiwemo kukatwa fedha zao.

“Nikimaliza ubunge nitarudi Ifakara, nitalima mpunga, nitaendesha bodaboda, lakini siwezi kuona haki yangu ikidhurumiwa. Niliendesha kampeni za uchaguzi mwaka 2015 nikiwa na shilingi milioni sita mfukoni, sikuchangiwa na chama, nilichangiwa na wananchi.

“Kila mwezi Wabunge wa Chadema tunakatwa Sh. laki tano, eti kuchangia mfuko wa chama wakati wa kampeni, fedha zilipofika bilioni nane na tulipohoji hizo fedha zipo wapi? Tukajibiwa uchaguzi ni harakati. Maamuzi ya kutoingia bungeni kwa wabunge wa Chadema haukuwa demokrasia wala makubaliano, kulikuwa na amri. Tulipohoji tulijibiwa kuwa hii ni amri tekeleza.

“Niliamua kurudi bungeni kwa sababu ya kufanya kazi za kibunge na siyo kutaka posho, Kama kuna mtu wanawaza posho basi mimi nilikuja bungeni kuwawakilisha wananchi,” amesema Lijualikali.

Aidha, Lijualikali  amemuomba Spika Job Ndugai endapo kuna uwezekano akahamia Chama Cha Mapinduzi ( CCM) yuko tayari hata kufanya kazi ya kufagia ofisi.

Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema yeye kama mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM kwa niaba ya chama chake anamkaribisha ndani ya CCM, Mbunge Peter Lijualikali na Mbunge yoyote anayetaka kujiunga na chama chochote anao uhuru na huu ndio wakati wake.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: