Afisa Usalama, Afya Mazingira na Ubora wa Kampuni ya Asas Cosmas Charles akimkabidhi Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko la Mashine Tatu, Japhary Sewando baadhi ya barakoa zilizotolewa kwa niaba ya mama lishe wa sokoni hapo kati barakoa 500 zilizotolewa kwa mama lishe wanaofanya biashara katika masoko matano ya manispaa ya Iringa.
Mmoja ya mama lishe wa soko kuu la Iringa akiwa amevaa barakoa zilizotolewa na kampuni ya Asas kwa mama lishe wote ndani ya manispaa ya Iringa


Afisa Usalama, Afya Mazingira na Ubora wa Kampuni ya Asas Cosmas Charles (kushoto) akiwa na baadhi wafanyabiashara wa soko la mashine tatu baada ya kuwakabidhi barakoa zilizotolewa na kampuni hiyo ambazo zimetolewa barakoa 500 kwa masoko matano. Picha na Denis Mlowe

NA FREDY MGUNDA. IRINGA

Katika kuendelea na mapambano dhidi ya kuenea kwa virusi vya corona nchini kampuni Asas yenye makao makuu mkoani Iringa imegawa msaada wa barakoa 500 kwa mama lishe wanaofanya biashara zao katika masoko matano yaliyoko manispaa ya Iringa kwa ajili ya kujinga na Virusi Vya Corona.

Msaada huo umetolewa kwa mama lishe hao ikiwa ni juhudi za kampuni hiyo kuungana na serikali katika kutokomeza kuenea kwa virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid 19 ambao umekuwa janga la dunia kwa sasa.

Akikabidhi msaada huo, Afisa Usalama, Afya Mazingira na Ubora wa Kampuni ya Asas Cosmas Charles  kwa niaba ya mkurugenzi wa uzalishaji wa kampuni hiyo, Ahmed Salim Abri alisema kuwa huo ni mwendelezo wa kampuni hiyo katika kusaidia jamii ambayo inahusisha mikusanyiko ya watu wengi zaidi ndani na nje ya mkoa wa Iringa

Alisema kuwa kampuni ya Asas imekuwa na utaratibu wa kusaidia jamii bila kuchoka kutokana hali za wananchi wengi sana kwa sasa kuhitaji msaada hivyo imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia jamii hasa katika suala zima la kupambana kuenea kwa virusi vya corona mkoani hapa na kuweza kutoa misaada mbalimbali kwa jamii yenye mikusanyiko kwa watu wengi.

Alisema kuwa msaada huo umewafikia mama lishe kutokana na kuwahudumia watu mbalimbali ambao wanatoka sehemu tofauti na kwa kuona changamoto yao baada ya kufanya utafiti na kubaini wengi wao wanauhitaji wa kupewa msaada wa barakoa ambazo ni bora.

Cosmas alisema alitoa wito kwa mama lishe hao kuhakikisha kwamba wanatumia barakoa na kunawa mikono kwa lengo la kujilinda wao na wateja wao wanaowahudumia kwa kuwa bila hivyo itakuwa rahisi endapo mmoja ana virusi hivyo kuvieneza kwa urahisi na kuwataka kuhakikisha wana nawa mikono kwa maji safi na sabuni za kutakasa mikono.
Alisema kuwa msaada huo umewafikia mama lishe wanaofanya biashara katika masoko ya Mashine Tatu, Kihesa, Soko la kisasa la Mlandege, Soko Kuu la Iringa na soko la Ipogoro ambapo kuna mwingiliano wa watu wengi wanaopata mahitaji sokoni hapo.

Aliongeza kuwa kampuni hiyo imekwisha toa msaada kwa umoja wa madereva daladala kwa kuwakabidhi vifaa kama ndoo maalum kunawia mikono na vitakasa mikono, barakoa zaidi ya 2000 kwa umoja wa madereva bajaji, msaada wa mashine ya kujifukuzia kwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa.

Kwa upande wao wenyeviti wa  masoko hayo wakizungumza kwa niaba ya mama lishe baada ya kukabidhiwa msaada huo walishukuru kampuni ya Asas kwa kuwa mstari wa mbele kurudisha faida kwa jamii na kutoa wito kwa makampuni mengine kuiga mfano wa kampuni hiyo kujitoa kwa jamii.

Walisema kuwa kampuni ya Asas inapata Baraka za MUNGU kwa kuwa imekuwa ikisaidia jamii hasa wenye uhitaji hali ambayo imewafanya kujijengea imani kubwa kwa wananchi ambao wamekuwa wateja wazuri wa kununua bidhaa zao kutokana na wao kuwathamini katika mazingira magumu.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko la Mashine Tatu, Japhary Sewando alisema kuwa wafanyabiashara wa soko hilo wamekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya kuenea kwa virusi vya corona katika soko hilo hivyo msaada huo umekuja wakati mwafaka kwa mama lishe hao hali ambayo wamefurahia na kushukuru kampuni ya Asas.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko kuu la mjini Iringa, Odilo Ngamilaga alisema kuwa kampuni hiyo imefanya jambo kubwa sana kwa mama lishe kuwapatia msaada huo ambapo wengi wao wanashindwa kumudu kutokana na hali halisi ya maisha kwa sasa.

Alisema kuwa kampuni hiyo imeunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kupambana dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona licha kwa sasa kupungua kwa kiasi kikubwa hivyo kutokana na kazi kubwa ya mama lishe wanahitaji kuwa na afya bora.
Share To:

Post A Comment: