SALVATORY NTANDU
Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga linamshikilia Mariamu Jumanne (23) Mkazi wa Mwadui ambaye ni  Mwanafunzi Chuo kikuu cha Dar es salaam kwa tuhuma za kuchapisha na kusambaza taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana wa COVID 19 hapa nchini.

Taarifa iliyotolewa leo na  Kamanda wa Polisi mkoani humo, ACP Debora Magiligimba kwa vyombo vya habari alisema kuwa Mariamu anatuhumiwa kuchapisha ujumbe wa maandishi kwenye mtandao wa Whatsapp  unaosema Tanzania ina wagonjwa 230 wa COVID 19  na Idadi ya wagonjwa  waliofariki ni wanne.

Alisema kuwa Machi 26 mwaka huu askari wa kikosi kazi cha mtandao kilifanikiwa kuona ujumbe kwenye mtandao huo wa kijamii wenye taarifa za uongo mtandaoni pamoja na kutoa takwimu za uongo.

Kamanda Magiligimba alisema kwa Mariamu alikamatwa  Aprili 9 mwaka huu Majira ya saa mbili Usiku eneo la Mwadui, Mtaa Wa Tabora, Kwenye Machimbo Ya Almasi Wilaya Ya Kishapu Mkoani humo baada ya kumufuatilia kwa njia ya mtandao

“Natoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Shinyanga kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii na kuacha kupotosha watu kuhusiana na ugonjwa wa COVID 19,”alisema Magiligimba.

Kamanda Magiligimba alisema kuwa  hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mariamu kuhusiana na makosa aliyoyafanya.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: