Kampuni ya uajiri na usimamizi wa rasilimali watu ya BrighterMonday Tanzania imeanzisha programu iitwayo ‘Umoja Wakati wa Shida’ inayotoa nafasi kwa waajiri (makampuni na watu binafsi) kutangaza kazi kwenye tovuti yao bure kwa kipindi cha miezi mitatu ijayo, wakati ambao taifa linakabiliana na janga la maradhi ya virusi vya Corona.

Kampeni hii inalenga kuwezesha uendelevu wa juhudi za makampuni na biashara kwa kuziwesesha kufanya udahili na kuajiri watendaji sahihi ili kuongeza ufanisi wakati na baada ya nyakati hizi za changamoto.

‘’Kwa miezi mitatu ijayo, tutatoa fursa kwa taasisi zinazotaka kuajiri wataalamu katika sekta mbalimbali kote nchini kutangaza bure nafasi za ajira katika tovuti yetu. Hii itawawezesha hospitali, vituo vya afya na watoa huduma nyingine muhimu walio mstari wa mbele katika kukabiliana na janga la virusi vya Corona (COVID-19) kuajiri wataalamu wenye vigezo kamilifu katika kipindi cha muda mfupi’’, anasema Mkurugenzi Mkuu wa BrighterMonday Tanzania, Bi. Reshma Bharmal-Shariff.

Chini ya programu hii, waajiri wataweza kuchakata kwa haraka mchakato wa uajiri kwa kutumia mbinu za kisasa zilizobuniwa na BrighterMonday Tanzania kama vile Zana ya Kupima Ufanisi wa Waajiriwa ambayo inapima ubora wa mwajiriwa na ujuzi unaohitajika kwa kazi anayoomba, zana hii hupima zaidi ya kile kilichopo kwenye wasifu (CV) ya mtahiniwa.

Vilevile, waajiri wataweza kuangalia alama za mtahiniwa pamoja kulinganisha na mahitaji ya kitaaluma na kiuzoefu kwa kutumia mfumo wa ufuatilaji wa maombi ya kazi ‘Application Tracking System’ (ATS) wa BrighterMonday Tanzania. Kupitia mfumo huu, mwajiri ataweza kulinganisha kwa urahisi ubora wa mtahiniwa, ujuzi na kiwango cha uzoefu.


‘Tupo kwa ajili yako jana, leo na hata kesho’- Timu ya BrighterMonday Tanzania inasema.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: