WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa lengo la serikali kuhamisha baadhi ya makao makuu ya wilaya ni kusogeza huduma karibu na wananchi.

Waziri Mkuu alisema hayo katika mji wa Mkata wilayani Handeni baada kuzungumza na wananchi baada ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigela kutoa ufafanuzi sababu za kuhamishia makao makuu ya Halmashauri ya wilaya ya Handeni kuhamishiwa katika mji wa Mkata.

Shigella alisema kuwa,makao makuu kuhamishiwa katika mji huo yamezingatia mambo mengi ikiwemo kuangalia kusogeza huduma kwa wananchi.

"Kuhamishia makao makuu ya Halmashauri ya wilaya ya Handeni tumeangalia mambo mengi tumeona kuwa wananchi kufuata huduma Mkata ni nafuu zaidi ambapo mtu anatumia gharama ya shilingi kati ya 3,000 na 5,000 wakati ukienda Kabuku unatumia shilingi 10,000,"alisema.

Alifafanunua kuwa baada kuangalia hilo,baraza la madiwani la halmashauri hiyo,walipiga kura kuona ni wapi panafaa kuwekwa makao makuu ambapo kati ya madiwani 27 waliopiga kura,26 walipendekeza makao makuu yawe Mkata.

Akiwa Kabuku,Waziri Mkuu alipata malalamiko kuwa makao makuu ya wilaya hiyo yamehamishwa kibabe bila ya wananchi  kushirikishwa na kutaka maelezo kuujua ukweli.

Akitolea ufafanuzi suala hilo,Waziri Mkuu amesema kuwa yeye hawezi kupinga maamuzi ya Makao makuu kuwa Mkata ikiwa yamezingatia matakwa na sera ya serikali ya kusogeza makao makuu karibu na wananchi.

Amesema kuwa tayari serikali imeshatoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya wilaya na serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi.

Sakata la mgogoro wa mvutano wa kujua wapi kujengwe makao makuu ya wilaya kati ya Mkata au Kabuku lilipelekea kwa aliyekuwa mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni,Ramadhani Diliwa diwani wa Kata ya Mgambo kujiuzulu nafasi yake mwaka 2018.
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: