Na John Walter-Manyara
Kutokana na kitendo cha Ubakaji na Mauaji kilichofanyika mapema mwezi machi 2020, katika kijiji cha Shaurimoyo kata ya Kisangaji wilayani Babati mkoa wa Manyara,wakazi wa maeneo hayo wameiomba serikali iwasaidie kuimarisha Ulinzi kwa kujengwa kituo kidogo cha Polisi kijijini hapo.
Hivi karibuni Katika kijiji cha Shaurimoyo, kata ya Kisangaji wilayani Babati mkoani Manyara, Kikongwe anaekadiriwa kuwa na zaidi ya miaka 80 Machi 8, 2020 alikutwa amefariki dunia baada ya kufanyiwa kitendo cha ukatili wa kubakwa na watu ambao bado hawajafahamika,  kisha kukatwa na kitu chenye ncha kali Vidole vya mikono na kuondolewa sehemu yake ya Unyayo, tukio ambalo wananchi wa kijiji hicho wamelihusisha na imani za Kishirikina.
Wakina mama wa Kijiji cha shaurimoyo wakizungumza na Kituo hiki, wanasema kwa sasa wanaishi kwa hofu kutokana na tukio hilo huku wakiamini kuwa serikali ikiwasaidia kujenga kituo kidogo cha polisi na kuwepo kwa askari kutasaidia kukomesha matukio ya iana hiyo.
Majirani wanasema kuwa mwili wa kikongwe huyo aliekuwa akiishi peke yake, ulikutwa ukiwa umekatwa sikio,Vidole vya mkono na kuondolewa nyayo zake.
Mwenyekiti wa kijiji cha ShauriMoyo Dismas Dodo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa wanakijiji alichukua hatua ya haraka ya kuwasiliana na  Jeshi la polisi kituo kidogo cha Magugu.
Diwani wa kata ya Kisangaji Adamu Ipingika akiwa Msibani, alikemea kitendo hicho na kuwataka wanakijiji kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili watuhumiwa waliofanya uhalifu huo waweze kubainika na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Aidha Mwenyekiti wa Kitongoji Kisangaji katika kata hiyo John Jakobo, alisema pia katika mwezi Machi,2020 mtoto wa miaka minne alibakwa katika kijiji hicho na mtuhumiwa mwenye miaka 30 ambapo kwa kushirikiana na wananchi walimkamata na kumfikisha katika kituo kidogo cha polisi Magugu.
Serikali na Mashirika yasiyo ya kiserikali  yamekuwa yakikemea vitendo vya ukatili na kutoa elimu kwa jamii  juu ya athari za vitendo hivyo, lakini bado matukio hayo yanaendelea kuripotiwa mara kwa mara katika mkoa wa Manyara na maeneo mengine hapa nchini.
Erick Lwongo ni mwanasheria kutoka shirika la kutetea haki za Binadamu la Haki madini lenye makao yake makuu  mkoani Arusha,anasema shirika linaendelea kutoa elimu kwa jamii na kukemea matendo hayo maovu.
Amesema suala la Ubakaji ni kosa la Jinai na adhabu yake haipungui miaka 30 kwa mujibu wa sheria za nchi ya  Tanzania na kwamba ubakaji sio njia sahihi ya mtu kumaliza haja zake.
Lwongo ameitaka jamii iweze kushirikiana katika kuwabaini wahalifu wa matukio ya ukatilo wa aina zote ili vyombo vinavyohusika viweze kuchukua hatua zinazostahili.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: