Wednesday, 11 March 2020

DC BABATI AUMIA WANAFUNZI KURUNDIKANA DARASANI,ATETA NA WANANACHI MAGUGU

 Mkuu wa wilaya ya Babati Elizabeth Kitundu akizungumza wakati wa mkutano huo


Na John Walter-Babati

WAZAZI katika Kata ya Magugu wilayani Babati Mkoani Manyara wametakiwa kujitolea ili kukamilisha ujenzi wa Madarasa katika shule ya Sekondari Magugu ili kuwasaidia wanafunzi wanaotoka umbali mrefu kwenda shule.

Akiongea na wananchi kijijini hapo mkuu wa wilaya ya Babati Elizabeth Kitundu, amewahimiza wazazi hao kuacha kuitegemea serikali katika kuwajengea shule.

Amesema kukosekana kwa madarasa,kumepelekea kuwepo kwa msongamano mkubwa wa wanafunzi kwenye darasa moja jambo ambalo sio rafiki kwa ufundishaji.

"Walimu wenyewe hawana ofisi,hakuna matundu ya vyoo ya kutosheleza,nipo chini ya Miguu yenu naomba mchange mlichonacho" aliongeza.

Amesema wanafunzi kwa sasa wanafaulu sana baada ya utaratibu wa serikali ya awamu ya tano wa Elimu bila Malipo, ambapo idadi ya wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza imeongezeka katika shule ya Sekondari Magugu hivyo kuwepo upungufu wa Madarasa.

Alisema kuwa wazazi wana jukumu kubwa katika kuhakikisha mwanafunzi anafanya vzuri katika masomo yake aua vibaya.

“Iwapo mnataka watoto wenu wasome vyema na katika mazingira bora, basi itabidi nyinyi kama wazazi mchangie katika kuimarisha na kuboresha mazingira ya elimu katika shule zetu na tuache kuitegemea serikali pekee,” aliongeza kusema.

“Serikali yetu imejitolea kuona kwamba shule zetu zinafikia viwango vinavyotakikina kimataifa ilituweze kuwapa watoto wetu mazingira mazuri ya kusomea,” alisema.

"Kwa hiyo mimi niwaombe Chonde chonde tuyajenge yale madarasa sita,tumalize,tuanze na vyoo na mipango mingine iendelee,hatutaki mtoto apate sifuri" alisema Dc Kitundu

Mchango kwa kila mkazi wa Magugu na vijiji vingine vya kata hiyo ni shilingi elfu 20,000.

Mkuu huyo wa wilaya amesema mara ya mwisho kufika katika shule hiyo michango ya wananchi ilikuwa ni shilingi Milioni 25 ambazo hazitoshi kwa idadi ya madarasa yanayohitajika.

Hata hivyo wananchi wanasema wapo tayari kuchangi pesa hiyo ila kwa masharti kuwa walipe kidogo kidogo hadi watakapokamilisha huku wakisaidiwa na wawekezaji waliopo katika maeneo yao.

Amesisitiza kuwa shule hiyo ni kwa ajili ya watoto wao na vizazi vijavyo, hivyo suala la kuchangia ni la lazima na sio hiari.

Wananchi hao wamesema wapo tayari kulipa michango hiyo ila wasitumie askari mgambo kwa kuwa wamekuwa wakiwanyanyasa.

Inaelezwa kuwa Kutokana na Miundombinu kuwa Mibovu katika shule ya Sekondari Magugu, kumechangia kwa kiasi kikubwa kufanya vibaya katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2019 kwa kushika nafasi ya pili kutoka Mwisho katika Halmashauri ya Babati, Wanafunzi 55 walipata alama 0 kati wanafunzi 174.

No comments:

Post a comment