Tuesday, 18 February 2020

WADAU WATAKA IWEPO SHERIA YA MIKANDA MAALUM KWENYE MABASI YA SHULE ZA AWALI/ MSINGI

    


               Na Abby Nkungu, Singida

Suala  la udhibiti wa ajali za barabarani limekuwa changamoto kubwa hapa nchini kwa miaka nenda-rudi licha ya juhudi  kubwa zinazofanywa na Serikali kupitia kikosi maalum cha askari  barabarani pamoja na wadau wengine mbalimbali ili kupunguza tatizo hilo linalosababisha vifo, majeruhi, ulemavu wa kudumu na uharibifu wa mali.

Ingawa zipo mbinu  nyingine nyingi zinazotumika kujaribu kupunguza ajali na madhara yake, lakini ripoti  ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia idara yake ya Global Health Observatory (GHO) ya mwaka 2015 kuhusu masuala ya usalama  barabarani,  inaonesha kuwa ufungaji sahihi wa mkanda huweza kupunguza madhara pindi ajali inapotokea kwa zaidi ya asilimia 50 kwa dereva na abiria wa viti vya mbele na zaidi ya asilimia 75 kwa abiria wa viti vya nyuma.

Hali hii ndiyo iliyofanya Sheria ya uvaaji mikanda kwenye magari kuenea kwa asilimia 87 Duniani kote wakati asilimia 13 iliyobaki ya nchi hazina Sheria hiyo kutokana na sababu mbalimbali.

Kwa  hapa nchini kwetu Tanzania, Sheria ya Usalama barabarani Kifungu 39 (11) na (12) X juu ya Makosa ya Usalama barabarani imeweka tozo la papo kwa hapo la shilingi elfu thelathini  (30,000/-) kwa kosa la dereva au abiria kushindwa kufunga mkanda wa gari anamosafiria. Hata hivyo, wadau wanaona kuwa sheria hii ina upungufu au kasoro kubwa kwa kuwa haijaainisha wala kutaja wazi mikanda hiyo ni kwa watu wazima tu au ni pamoja na mabasi ya watoto wa shule; hasa Shule za Awali.

Katika  mahojiano maalum na Mwandishi wa makala hii, baadhi ya wazazi na walezi wanasema kuwa  upungufu huo wa Sheria ya Usalama Barabarani  ni kikwazo kikubwa katika suala zima  la utekelezaji wa dhana ya ulinzi  na usalama wa mtoto; hasa wenye umri chini ya miaka minane. Mmoja wa wazazi hao, Juma Athumani mkazi wa Unyankindi mjini Singida anasema kuwa ukosefu wa mikanda maalum ya kujifunga watoto kwenye viti vya mabasi ya wanafunzi wa shule za awali ni hatari kubwa  kwa kundi hilo na linaathiri  juhudi za ulinzi na usalama kwa mtoto.

"Bwana Mwandishi hebu fikiria, kama tafiti  zinaonesha kuwa ufungaji wa mikanda unapunguza madhara wakati wa ajali kwa 50% hadi 75% halafu  sisi tunapakia  watoto wetu wadogo kwenye magari yasiyo na mikanda, huoni hiyo ni hatari kubwa" alisema Athumani na kuhoji "sijui ni kwa nini Serikali haichukui hatua stahiki kwa wamiliki wa mabasi haya?”.

Naye Rose Mwiko mkazi wa  Karakana mjini Singida anasema kuwa wengi  wa wamiliki wa mabasi ya kubeba wanafunzi wamechukulia upungufu wa Sheria ya usalama barabarani kuwa ngao ya kuleta magari yasiyokuwa na mikanda maalum kwa ajili ya watoto.

"Kwa kawaida watoto hawa wadogo tunaowapeleka chekechea wakiwa na miaka minne huwa wanachoka sana kwa kuamka kila siku asubuhi; hivyo huwa tunawapandisha kwenye mabasi wakiwa na uchovu na usingizi, halafu hakuna mkanda wa kumfunga wakati baadhi ya mabasi watoto hujazwa hadi wanapakatiana" alisema na kuongeza kuwa "Basi tu huwa  tunaomba Mungu  awaepushe na suala la ajali". Wanasema  kuna haja kwa Serikali kuiangalia upya Sheria hiyo ya usalama barabarani na  kuifanyia marekebisho ili kuweka kipengele cha  kuwalazimisha wamiliki wa shule za Awali na Msingi kuwa na mabasi yenye mikanda maalum kwa watoto wadogo; hasa wasiozidi miaka 10, kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani.

"Ujue viongozi  wetu wakati mwingine huwa wanahitaji kukumbushwa mara kwa mara ili wafanye jambo. Sijui wanasubiri nini kitokee ndio wachukue hatua kwani ajali ya Shule ya Lucky Vincent mkoani Arusha miaka mitatu iliyopita ambapo watoto 30 walipoteza maisha, ilikuwa ni fundisho tosha kwa Mamlaka zinazohusika. Watoto wadogo kukosa mikanda kwenye gari ni hatari zaidi kuliko kuhimiza rangi ya mabasi hayo yapakwe rangi ya njano" alisema mzazi mwingine, Neema Lameck wa Mtipa nje kidogo ya mji wa Singida.

Ofisa Usalama barabarani Mkoa wa Singida (RTO), Edson Mwakihaba anakiri kuiona changamoto hiyo na hatari iliyopo katika suala  la ulinzi na usalama wa mtoto barabarani lakini anasema hana mashiko ya kisheria kulihimiza. "Katika mkoa wangu, hakuna shule hata moja ya awali wala msingi yenye mabasi yaliyo na mikanda maalum kwa ajili ya wanafunzi kujifunga kwenye viti vyao pindi wanaposafiri kwenda shuleni " alisema.
"Mabasi mengi yaliyopo kwenye shule hizo yalikusudiwa kusafirisha abiria watu wazima na viti ni vikubwa; hivyo mikanda iliyopo haiwezi kutumika kwa watoto wadogo walio chini ya umri wa miaka minane. Lakini pia watoto hujazana mno kiasi kwamba hata kama kungekuwa na mikanda maalum haingewezekana kila mmoja kujifunga" alifafanua na kuongeza kuwa jambo lenyewe hilo linaonekana kama vile ni geni nchini.

"Kutokana na sheria kukaa kimya juu ya suala hili, utaona kuwa hata wamiliki wa mabasi ya wanafunzi walio chini ya umri wa miaka 8 hawalazimiki kuwa na usafiri wa aina hiyo wala sisi hatupaswi kuwakamata kwa kosa hilo" alisema Mwakihaba huku akifafanua kuwa kati ya mabasi zaidi ya 30 yanayosafirisha wanafunzi  wa shule za awali  na msingi mkoani Singida hakuna hata moja lenye mikanda maalum kwa watoto kwenye viti vyake.

Hata hivyo, Mwongozo wa usajili wa shule za awali na msingi wa mwaka 1982 unaeleza juu ya mahitaji muhimu kabla ya kuanzisha Taasisi za aina hiyo kuwa ni  pamoja na kupata kibali cha kujenga majengo, kuwa na fedha za kuanzisha mradi huo na nakala ya hati ya uthibitisho wa kumiliki ardhi iliyotolewa kwa  ajili ya matumizi ya shule inayotambulika kisheria.

Mahitaji mengine ni pamoja na michoro ya majengo ya shule inayoonyesha vipimo kwa kuzingatia viwango vya Wizara na Elimu, Ramani ya shule inayoonyesha mpangilio wa majengo na viwanja vya michezo, cheti cha usajili wa Kampuni, Shirika, Umoja, NGO iwapo shule ni ya Jumuia na Katiba.

Pamoja na Mwongozo huo kuweka masharti na vigezo muhimu vya kuanzisha shule za msingi na  awali  juu ya majengo ya utawala, madarasa, vyoo, uzio wa shule na mahitaji mengine lukuki, lakini suala la usafiri unaotumika kuwapeleka shule na kuwarejesha nyumbani watoto halijagusiwa hata chembe.
Swali  linabaki  kuwa: Je, bado suala  hilo sio muhimu kuwekwa kama moja ya masharti muhimu ili kuhakikisha ulinzi na usalama wa mtoto; hasa katika kipindi hiki ambapo shule nyingi  za awali zinazochukua watoto walio chini ya miaka sita zina mabasi yasiyokuwa na mikanda?
Ni imani yangu kuwa katika Serikali hii sikivu ya Awamu ya Tano ya Rais Dk John Magufuli, suala hili litaangaliwa kwa jicho la pekee kama sio kuwekwa kwenye Sheria ya Usalama barabarani basi angalau kwenye Mwongozo wa Usajili wa shule au sehemu nyingine yoyote ili kulinda usalama wa watoto wanapokwenda shule na kurudi nyumbani.

No comments:

Post a comment