Na WAMJW - Morogoro

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,  Jinsia, Wazee na Watoto leo amezindua Kampeni ya Kipepeo Mkoani Morogoro.

Kampeni hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (NACP) na Taasisi ya Benjamin William Mkapa.

Akizungumza Waziri Ummy amesema kampeni hiyo inalenga kuwasaidia wanafunzi hasa wa kike kujitambua, kujiamini na kuongeza bidii ya kujenga ndoto zao sambamba na kuwapatia mbinu za namna ya kupambana na changamoto mbalimbali za kimaisha, kimasomo na vishawishi vinavyoweza kuwapotezea mwelekeo na kushindwa kufikia ndoto zao.

"Wizara ikishirikiana na taasisi na wadau wa masuala ya afya inalenga kuifanya Kipepeo kuwa kampeni kubwa zaidi ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi wa rika balehe wanaosoma shule za sekondari.

"Kuwafikishia elimu kuhusu maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), athari za mimba za utotoni, matumizi sahihi ya ARV kwa wale walioathirika tayari sambamba na kueneza elimu dhidi ya unyanyapaa," amesema Waziri Ummy.


Naye, Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa amesema Kampeni ya Kipepeo itafanyika kwenye jumla ya mikoa kumi (10).

Ametaja vigezo vya kuchagua Mikoa husika ni viwili kwanza wamezingatia  mikoa yenye kiwango cha juu cha maambukizi ya VVU kwa kundi linalolengwa, pili ni mikoa yenye kiwango cha juu cha mimba za utotoni.

"Mikoa hiyo ni pamoja na Mbeya, Iringa, Njombe, Mwanza, Dodoma, Tanga, Arusha, Mtwara, Morogoro na Singida," ameitaja.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro  Loatha Sanare amesema Mkoa wake unaunga mkono Kampeni hiyo.

"Kwa sababu, kupitia kampeni kama hizo Mkoa umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), athari za mimba za utotoni, matumizi sahihi ya ARV kwa wale walioathirika tayari sambamba na kueneza elimu dhidi ya unyanyapaa," amesema.

MWISHO
Share To:

msumbanews

Post A Comment: