Thursday, 23 January 2020

NIMR YATENGA MILIONI 800 TIBA YA MITISHAMBA NCHINI


Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kituo cha Muhimbili Prof. Sayoki Mfinanga akieleza jambo wakati wa kikao na Maafisa Habari wa Wizara ya Afya na Taasisi zake pamoja na Waandishi wa Habari kilichofanyika katika ofisi za Taasisi hiyo Muhimbili, Jijini Dar es Salaam.
Msanifu wa Maabara ya NIMR-Muhimbili Said Omary akielezea namna vimelea  vya ugonjwa wa kifua kikuu vinavyokuzwa kwenye Maabara hiyo ya utafiti.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Prof. Yunus Mgaya akisisitiza jambo wakati wa kikao na Maafisa Habari wa Wizara ya Afya na Taasisi zake pamoja na Waandishi wa Habari kilichofanyika katika ofisi za Taasisi hiyo Muhimbili, Jijini Dar es Salaam.
...........................

TAASISI ya Taifa ya Utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR) imesema ipo mbioni kusimika mitambo ya kisasa itakayosaidia kuzalisha dawa za mitishamba kutoka miti dawa ili kukabiliana na magonjwa mbalimbali nchini .mwandishi Andrew Chale anaripoti

Mkurugenzi wa NIMR, Profesa Yunus Mgaya akizungumza wakati wa ziara ya 'Tumeboresha Sekta ya Afya' inayoendeshwa na maafisa habari waandamizi wa Wizara ya Afya na Taasisi zake.

Maofisa habari hao wapo katika ziara ya Kampeni iitwayo Tumeboresha Sekta ya Afya ambayo inalenga kuonesha mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Pombe Joseph  Magufuli

Alisema Serikali ya awamu ya tano kupitia Wizara ya afya imetoa fedha shilingi Milioni 800 ambazo zitasaidia kununulia mitambo na kukarabati eneo itakaposimikwa mitambo hiyo.

"NIMR tupo mbioni kuleta mitambo kutoka China mitambo ambayo itatoa uwezo wa kuzalisha dawa kutoka kwenye miti dawa kwa ajili ya kuongeza uwezo wa kukabiliana dhidi ya magonjwa mbalimbali ambayo yanawagusa wananchi."

"Watalaam wetu tayari wameshaenda China kujifunza na pia wametembelea kampuni za mitambo hiyo ya kisasa na tumejiridhisha.

Mtambo mmoja unagharimu kati ya shilingi za kitanzania Milioni 500 hadi milioni 600 hivyo milioni 800 zitatosha kabisa kukamilika zoezi zima" alisema.

Pia alisema kuwa, dawa hizo zitatokana na miti dawa mbalimbali ikiwemo na kwa Waganga hapa nchini.

"Sisi tutatengeneza dawa kutokana na asili ya miti dawa.
 Tunachokifanya ni kutafiti. Baada ya kwenda kwa Mganga ambaye atakumiminia kwenye kikombe, Sisi tutakachokuambia ni kuwa dawa hiyo inamchanganyiko wa kiambata fulani na utaitumia kwa kiwango fulani." Alisema.

Aidha, alisema katika tiba ya mitishamba duniani inatumika kwa wingi katika nchi mbili pekee ikiwemo China na India.

"China na India kuna Hospitali kabisa zinatibu kwa kutumia dawa za mitishamba na Nchi ya Korea pia" Alisema Profesa Mgaya.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa NIMR kituo cha Muhimbili, Profesa Sayoki Mfinanga  alieleza kuwa miongoni mwa mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya awamu ya tano ni pamoja na kuongezeka kwa tafiti kutoka 10 hadi 20 kwa mwaka.

"NIMR-Muhimbili  tumefanikiwa kufanya tafiti mbalimbali kwenye magonjwa ya Kifua kikuu, Vimelea vya Ukimwi na Magonjwa yasiyoambukiza (Non Communicable Diseases).

"Uwezo wa kituo wa kufanya tafiti umeongezeka kutoka wastani wa tafiti kubwa 10 kwa mwaka kwenye miaka ya nyuma ya 2010 mpaka  wastani  wa tafiti kubwa 20 kwenye miaka ya kuanzia 2017." Alisema Profesa Mfinyanga.

Ambapo alibainisha kuwa, miongoni mwa tafiti hizo ni pamoja zile za huduma za kudhibiti Ukimwi na Kifua Kikuu.

"Tafiti hizi kupitia NIMR-Muhimbili zimechangia kuboresha au kutoa taarifa zilizoboresha huduma za kudhibiti UKIMWI na kifua kikuu.

"NIMR-Muhimbili imekamilisha utafiti uliotathimini mkakati tiba kwa kupunguza vifo kwa wagonjwa  wenye  maambukizi ya fangasi (Cryptococcus Neofroman)  na kusababisha homa ya Uti wa mgongo (Cryptococcal meningitis) kwa wagonjwa walioathirika na Ukimwi.
 Utafiti huu umehusisha wagonjwa 721 toka Tanzania,  Malawi, Zambia,  na Cameroon. "Alisema profesa Mfinanga.

Aidha, katika ziara hiyo pia wanahabari na maafisa hao wa Wizara ya Afya waliweza kitembelea Maabara kubwa ya NIMR -Muhimbili  na kujionea jinsi inavyofanya kazi huku wakishuhudia vifaa na mashine za kisasa kabisa zenye ubora na ufanisi wa hali ya juu.

NIMR ilianzishwa kwa sheria ya bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Namba 23 ya mwaka 1979.
NIMR ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto huku kazi yake kubwa ni pamoja na kufanya utafiti, inaratibu, inakuza na kusimamia
tafiti za afya zinazofanyika nchini na kukuza matumizi ya matokeo ya tafiti hizo.

Ambapo pia hadi sasa ina idara ya tafiti za Tiba Asili ambayo jukumu lake ni kufanya utafiti juu ya dawa za miti-shamba,
ambazo nyingine zimekuwa zinatumika miaka mingi na bibi na babu zetu.


No comments:

Post a comment