NA ANDREW CHALE

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa tamasha kubwa la kukuza na kuendeleza Utalii la LAMADI UTALII FESTIVAL.

Mwenyekiti wa Kamati  wa Tamasha hilo, Mkuu wa Wilaya ya Busega Bi. Tano Mwera amesema tamasha hilo la siku nne, litazinduliwa rasmi Desemba 29 mwaka huu na Naibu Waziri wa Maliasili katika viwanja vya shule ya Itongo, Lamadi.

"Mhe. Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu atazindua rasmi tamasha letu hiyo Desemba 29.

Pia kutakuwa na shughuli mbalimbali za tamasha ikiwemo biashara za wadau mbalimbali ambalo watu wanakaribishwa na hakuna kiingilio ni bure" alisema Mkuu wa Wilaya Bi. Tano Mwera.

Tamasha hilo pia litakuwa na shughuli za safari  za kitalii ikiwemo ya kwenda Hifadhi ya Serengiti kwa malipo ya gharama nafuu.

"Tarehe 1.1.2020 kuna tukio la kwenda hifadhi ya Serengeti na gharama ni Tsh. 55000, kwa kila Mtanzania lakini watoto 10 wa mwanzo wao watalipiwa Tsh. 50,000 pekee kama ofa. Gharama hiyo itajumlisha  usafiri wa kutoka na kurudi Lamadi, ada ya kiingilio, chakula cha mchana, vinywaji laini.

Nafasi ni chache kwani idadi ni watu 30, safari ya siku moja kutoka saa 12 alfajili na kurudi Saa 12 jioni." Alieleza DC Tano Mwera.

Pia shughuli nyingine ni Utalii wa kwenye boti 'Boat Cruising'  ambapo gharama itakuwa Tsh. 10,000 kwa Mtanzania na muda ni masaa matatu kwenye maji.

"Desemba 31 tutakuwa na Safari za Boat itaanza Saa tatu Asubuhi.  watapata wasaa kuzunguka kwenye boti ndani ya masaa matatu na kurejea.

Pia tutakuwa na Biking, hii gharama yake ni Tsh. 5000 kwa kila Mtanzania ikijumuisha kukodi baiskel kwa nusu siku pamoja na maji ya kunywa.

"Desemba 30, tutakuwa na Biking itaanza saa 12 asubuhi hadi mida ya saa 5 asubuhi. Kuzunguka mji na baiskeri ni Utalii  mzuri lakini pia ni mazoezi yatakayoimalisha afya zetu kwa tunatarajia kuwa na watu wengi sana" alieleza DC Tano Mwera.

Mbali na shughuli hizo za Utalii, Wananchi watapata kuona shughuli mbalimbali ikiwemo burudani, michezo pamoja na kufanya manunuzi ya vitu.

"Unakosaje Lamadi Utalii  Festival.!! Vyakula vya asili, Nyama choma,Uchomaji wa samaki (Sato Corner).

Wasanii wa kila aina. Wachoraji, wasusi, wachonga vinyago na mengine mengi." Alieleza DC Tano Mwera.

Aidha, katika tamasha siku ya mkesha wa Mwaka Mpya kutakuwa na usiku maalum wa 'Karaoke Night' ambao watu mbalimbali watapata wasaha wa kuimba nyimbo mbalimbali na kufurahia pamoja mwaka mpya.

Tamasha hilo mwaka huu ni la kwanza na kudhaminiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na wadau wengine mbalimbali huku likiwa na Kauli mbiu ya "Utalii wa Ndani Unawezekana".

 Mwisho.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: