Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mhe. Stephen Masele, amempongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anyoifanya ya kusimamia nidhamu ya fedha na watumishi wa umma, hali ambayo imesukuma kutekelezwa kwa miradi mingi ya maendeleo.

Masele ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP) amebainisha hayo leo Desemba 27, 2019, katika mfululizo wa ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo lake la Shinyanga mjini na kuzungumza na wananchi wa Kata ya Kolandoto Manispaa ya Shinyanga.

Amesema kutokana na kazi nzuri ambayo anaifanya Rais John Magufuli ya kusimamia nidhamu ya fedha na watumishi wa umma, kazi yake imeonekana, ambapo miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa, kitendo ambacho kimezidi kukiimarisha chama cha Mapinduzi na kuwa na imani kwa wananchi.

Masele amesema kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Rais John Pombe Magufuli uchaguzi mkuu mwaka  2020 CCM itashinda kwa kishindo kama ilivyofanyika uchaguzi Serikali za mitaa mwaka 2019.

“Nampongeza Rais John Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya ya kusimamia nidhamu ya fedha, na mimi Mbunge wenu nitaendeleza kasi hii ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama anavyofanya Rais wangu, nadhani mnaiona Shinyanga jinsi ilivyobadilika kimaendeleo kwa sasa ndani ya miaka yangu tisa ya ubunge, ambapo kuna barabara za lami kila mtaa, pamoja na taa zake,”amesema Masele.

“Huduma za afya  nimeziboresha, elimu, maji yapo, ujenzi wa madaraja, na sasa hivi tumeshatenga tena kilomita 18 za ujenzi wa barabara mpya kwa kiwango cha lami tofauti na hizi Kilomita 13 ambazo zimejengwa, yaani nataka Shinyanga uwe  Mji wa kisasa ninaposema Shinyanga ni Paris ya Tanzania nina maana kubwa ya kuifanya shinyanga kuwa pahala pazuri pa kuishi kama ilivyo miji ya kisasa. Na  uwezo huo ninao,”ameongeza Masele.

Pia ameahidi kuendelea kumalizia baadhi ya ahadi zake ambazo amebakiza kwenye baadhi ya maeneo, huku akitoa mifuko ya Saruji 150 ili kumalizia majengo ya ujenzi wa Zahanati ya Mwanubi, ambapo wamepatiwa mifuko 100 ya Saruji, pamoja na zahanati ya  Mwamagunguli Mifuko 50 zote za Kata ya Kolandoto ili kusogeza huduma za afya kuwa karibu na wananchi.

Nao baadhi ya wananchi wa Kata hiyo ya Kolandoto Manispaa ya Shinyanga akiwemo Naimani Ngeleja, wamempongeza Mbunge Masele kwa kazi nzuri ambayo ameifanya kwenye uongozi wake, ikiwa ahadi nyingi amezitekeleza huku wakiomba awasaidie kupeleka huduma ya umeme wa REA kwenye baadhi ya vijiji ambavyo havijapitiwa na mradi huo.

Aidha kwa upande wake Diwani wa Kata  ya Kolandoto Agnes Machiya, akisoma taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya  CCM kuanzia (2015-19), amesema asilimia 90 ya ahadi zimeshatekelezwa, ikiwamo ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja, elimu, Afya pamoja na miradi ya maji safi na salama.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: