Kusuasua kwa ukamilishaji wa ujenzi wa baadhi ya miundombinu katika Chuo cha Ualimu Mpuguso, Mkoani Mbeya unaotekelezwa na mkandarasi Lukolo Construction Company umepelekea Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako kutoa agizo kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo kusimamia kwa karibu ukamilishaji wa kazi hiyo ili majengo hayo yaweze kutumiwa na walimu tarajali. 

Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo mara baada ya kukagua mradi huo na kukuta ukitekelezwa kwa hali isiyoridhisha na katika baadhi ya maeneo  kuwa chini ya kiwango.

Amesema mkandarasi huyi pamoja na kushindwa kukamilisha kazi yake kwa wakati  aliepewa muda zaidi ili kukamilisha kazi hiyo lakini bado hajakamilisha hivyo  kupelekea chuo kushindwa kutumia  miundo mbinu na Serikali kuchelewa  kufikia malengo yake ya uboreshaji na upanuzi wa Chuo hicho.

"Naelekeza mradi huu ukamilike ifikapo Desemba 30 tena kwa ubora kama ilivyopangwa  hivyo Katibu Mkuu afuatilie kwa karibu kazi hii  na makandarasi akishindwa kukamilisha mchukulie hatua," amesema Ndalichako

Kiongozi huyo alisema kwa mujibu wa makubaliano mapya baada ya kurudishwa kazini ni kukamilisha kazi hiyo Desemba 30, 2019 lakini hata sasa haonekani kuwepo eneo la mradi na hakuna kinachoendelea.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa mbeya Albert Chalamila amemweleza waziri kuwa mkandarasi huyo asipokamilisha kazi hiyo kwa muda uliopangwa atachukuliwa hatua na kuwa kama Mkoa watafuatilia pia utekelezaji wake kwa karibu.

 Katika hatua nyingine  Mkuu wa Mkoa wa Mbeya pia amemwomba waziri wa elimu kukipatia Chuo hicho  gari ili kusaidia katika huduma mbalimbali jambo ambalo Waziri aliridhia na kusema kuwa tayari  Wizara imenunua magari kwa ajili ya  vyuo vya ualimu ambavyo havina huduma hiyo.

Nae mkuu wa chuo cha ualimu Mpuguso Dorothy Mhaiki ameishukuru Serikali kwa namna inavyoboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika chuo hicho na kuomba kukarabati maeneo mengine yaliyobakia kwa kuwa bado kuna uhitaji ikiwa ni pamoja na kusaidia kupatikana watumishi wa kudumu Upande wa walinzi na wapishi ili kupunguza gharama ya uendeshaji.

Ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu katika Chuo cha Ualimu Mpuguso ni  sehemu ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi na ukarabati wa miundo mbinu katika Chuo hicho ambao umegharimu  kiasi cha sh bilioni 10 unaotekelezwa na serikali ya Tanzania na ile ya Canada.

Mradi huo umetekelezwa na kandarasi mbili Salem Construction Ltd ambao wamekalilisha kazi zao kwa ubora na majengo kuanza kutumika na Lukolo Construction Company ambao bado kazi yao haijakamilika.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: