Tuesday, 12 November 2019

WAZIRI KALEMANI AWATAKA WANANCHI KUTOJENGA KWENYE NJIA ZA UMEME MKUBWA Na Veronica Simba -Manyara

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ametoa rai kwa wananchi wote kutojenga nyumba za aina yoyote kwenye njia za umeme mkubwa kwani ni hatari kwa maisha yao hivyo hairuhusiwi kisheria.

Akiwa katika ziara ya kazi wilayani Mbulu, Mkoa wa Manyara, Novemba 11, mwaka huu, Waziri alisisitiza suala hilo kwa nyakati tofauti katika mikutano ya hadhara maeneo mbalimbali na akalazimika kuzungumza na baadhi ya wananchi walioanzisha ujenzi kwenye njia hizo katika kijiji cha Maretadu Chini.

“Wito huu ni kwa wananchi wote Tanzania nzima; hairuhusiwi kujenga nyumba kwenye njia za umeme mkubwa. Pia, nawaagiza Mameneja wa TANESCO nchini kote kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi juu ya suala hili ili waelewe athari zake.”

Katika hatua nyingine, Waziri aliwasha umeme katika vijiji vya Tumati na Maretadu Juu ambako pamoja na mambo mengine, alisema kuwa kipaumbele cha kuunganisha umeme vijijini ni kwa Taasisi za umma, hivyo akawasisitiza viongozi, ngazi za wilaya na vijiji, kutenga fedha kwa ajili ya kazi husika.

Kuhusu idadi ya vijiji vilivyo kwenye mpango wa kupelekewa umeme kupitia miradi ya REA, Waziri alieleza kuwa vijiji vipya 11 vimeongezwa katika 12 vilivyokuwa kwenye mpango wa awali na pia TANESCO watashusha umeme katika vijiji vingine 15 kupitia Mradi wa Miji-Vijiji (Peri-Urban).

“Kwa ujumla, mpaka Mradi utakapokamilika Juni 2021, tutakuwa tumepeleka umeme katika vijiji 54 badala ya 12 ambavyo ni sawa na asilimia 75.2 ya vijiji vya Mbulu Vijijini.”

Alisema, vijiji 22 vitakavyobaki vitaanza kupelekewa umeme Februari mwakani na kwamba hadi kufikia Juni 2021, vijiji vyote vitakuwa vimeshafikiwa na umeme.

Aidha, Waziri Kalemani alitoa maagizo kwa Mameneja wa TANESCO nchi nzima, kupokea pesa za wateja wanaoomba kuunganishiwa umeme vijijini na wawapatie huduma hiyo pasipo kujali kama wako kwenye wigo au la.

“Ilimradi transfoma imeshafika kwenye kijiji husika; mwombaji apokelewe pesa yake ambayo ni shilingi elfu 27 tu na aunganishiwe umeme.”

Akizungumzia hali ya upatikanaji umeme mkoani Manyara, Waziri Kalemani alisema kuwa ni ya kuridhisha na inaendelea kuimarika. Alisema, mahitaji ya umeme kwa mkoa mzima ni megawati 18.2 wakati uzalishaji ni zaidi ya megawati 34 hivyo megawati 16 ni ziada.

Aliwapongeza TANESCO mkoani humo kwa utendaji kazi mzuri lakini akawataka waendelee kufanya marekebisho mahali ambapo bado kuna hitilafu ndogondogo zinazosababisha baadhi ya maeneo kukosa umeme.

Hata hivyo, Waziri alifafanua kuwa, inapotokea mahala hakuna umeme unakuwa umezimwa kwa sababu maalum zinazohusisha kufanya matengenezo kwa ajili ya kuimarisha mitambo au kutokana na hitilafu.

Waziri aliwasisitiza watendaji wa TANESCO kutoa taarifa kwa wananchi wa eneo husika pale wanapozima umeme kwa sababu yoyote ile pamoja na kueleza bayana huduma itarejeshwa baada ya muda gani.

Katika ziara hiyo ya siku moja, Waziri pia alitembelea kijiji cha Haydom ambako alizungumza na wananchi na kuwahakikishia kuwa Serikali inaendelea kuboresha huduma za upatikanaji umeme wa uhakika kwa wananchi.


No comments:

Post a comment