NA ANDREW  CHALE,

MIKOA ya pembezoni mwa Nchi ikiwemo ya Kanda ya Magharibi, Kanda ya Ziwa na ile ya Kaskazini imeripotiwa kuwa  kinara wa dawa duni za binadamu na mifugo, vifaa tiba na vitendanishi ambavyo havikusajiliwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA).

Akitangaza matokeo ya operesheni maalum  ya dawa, vifaa tiba, vitendanishi, dawa asili na tiba mbadala, mbele ya waandishi wa habari mapema leo Jijini Dar e Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Bw. Akida Khea   alisema katika zoezi hilo Wilaya zaidi ya 33 katika mikoa 20 wameweza kukamata dawa bandia aina saba zenye thamani ya fedha za kitanzania Tsh. 12,495,500.

Dawa hizo bandia ni pamoja na  Sonaderm Cream toleo namba A1912 na A1758, Gentrisome cream (namba GNTRO X030), Sulphadoxine Pyrimethamine (ilikuwa na namba ya kughushi TAN)

Pia dawa zingine ni  ALPRIM (Sulfamethoxazole 400mg + Trimethoprim 80mg tablets (namba  6L74) ambapo kiwanda cha Elys Pharmaceutical cha nchini Kenya kinachozalisha dawa yenye jina kama hilo kimethibitisha kuwa dawa hizo ni bandia.

Bw. Khea alizitaja dawa zingine kuwa ni pamoja na Homidium Chloride,  Cold cap ambapo dawa halisi yake ilitambuliwa  kama COLDCAP, na dawa nyingine bandia ni dawa ya mifugo aina ya TEMEVAC NDV strain 1&2  ambayo ni chanjo ya kuku  kwa ajili ya ugonjwa wa mdondo.

“katika dawa hizo, uchunguzi wetu baada ya kuzibaini tuliweza kuwasiliana nawamiliki wa dawa husika ambapo waliweza kututhibitishia kuwa ni bandia na zingine zimegushiwa maandishi” alisema Khea.

 “Tumebaini mikoa  iliyo pembezoni ikiwemo Kigoma kubainika kuwa na dawa nyingi bandia pamoja na Mwanza. Lakini pia mikoa ya Kaskazini ikiwemo Arusha na Kilimanjaro nayo imebainika kuwa na wingi wa dawa hizo” alisema  Kaimu Mkurugenzi huyo wa TMDA, Akida Khea.

 Katika tukio hilo TMDA waliwashirikisha mamlaka mbalimbali wakiwemo Jeshi la Polisi, Msajili wa Baraza la dawa asili na tiba mbadala pamoja na TAMISEMI.

Nae Mrakibu wa jeshi la Polisi kutoka Makao makuu ya upelelezi kitengo cha Interpool,  Alekunda Urio  amesema jeshi hilo linafuatilia kwa karibu na wahusika wote ambao wamebainika katika kuingiza ama kusambaza watachukuliwa hatua.

"Wajibu wa jeshi la Polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao. Usalama wa raia ni pamoja na afya za wananchi sisi kama jeshi la polisi kwa pamoja tunahakikisha usalama wa raia unalindwa na wahusika watafikishwa kwenye vyombo vya sheria uchunguzi ukikamilika" alisema Bi Alekunda Urio.

Mwisho.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: