Friday, 29 November 2019

CHUO KIKUU RUKWA NA MKAKATI WA KUWAINUA WAKULIMATasnia ya kilimo inao wajibu mkubwa mno wa kuwalisha ili kuhimilisha uhai wa watu wapatao billioni tisa ifikapo mwaka 2040 kwa makadirio ya wanazuoni.

Na ili kuweza kufanikiwa katika azma hiyo kilimo ni shurti kiongeze uzalishaji wa chakula katika miaka arobain ijayo kwa kiasi ambacho kinazidi ongezeko lililokwisha kufanyizwa katika miaka 10,000 iliyopita kwa ujumla (in the past 10,000 years combined).

Yapo mambo makubwa matano yanayochukua nafasi kubwa ya majadiliano na uchambuzi duniani kote kwa sasa kuhusiana na kilimo:

La kwanza ni ufahamu na ukubalifu wa wajibu wa bei za chakula.

Wakati bei za vyakula kwa upande mmoja zikizungumzwa kuwa zinachochea, mfumko wa bei za bidhaa nyingi ikiwemo nishati katika nchi nyingi, ni wakati huo huo ambapo bei za vyakula hazitizamwi wala kupendekezwa kama kivutio na kichocheo cha ongezeko la uzalishaji kukidhi mahitaji.

Kuwezesha wakulima kuzalisha chakula kingi na wakati huo huo kukifikisha katika masoko na kuwalisha wafanyakazi zingine za viwandani, migodini, na huduma nyinginezo muhali kwa ubora wake na kwa bei wawezazo kumudu ni wajibu mkubwa wa madaraka zote na uongozi wa dunia yetu kwa vitendo na si kwa siasa za majukwaani.

Pili, wajibu wa wakulima wadogo wadogo kama wadau muhimu na nguvu ya uzalishaji mkubwa wa kibiashara kama vile ilivyo kwa mashamba makubwa ya kikabaila ni suala linalojadiliwa kama njia ya kutegemeza amani ya kudumu  hususan katika suala nyeti kama ardhi na umiliki wake.

Watetezi wa ukabaila wanadharau uzalishaji wa mashamba madogo na kuyaita vipande  vya kujikimu visivyo na tija, jambo ambalo halina ukweli kwani kinachohitajika ni sera zilizo bora pamwe na usimamizi wa kuviwezesha vipande hivyo kuwa  shamba moja kubwa lenye umiliki wa kuhimilisha amani ya kudumu angalau kwa nyakati tulizo nazo.
     
La tatu na ambalo linajikita moja kwa moja katika kuazimia kuanzisha Chuo Kikuu cha Rukwa ni lile la wajibu wa sayansi na teknolojia na ubunifu utokanao; kwamba ni wakati ambao vinahitajika kuliko wakati wowote uliotangulia kuwezesha uzalishaji wa chakula cha kutosha wakazi wa dunia na kutafiti yale yanayopaswa kufanyika kutegemeza wakati ujao kwa chakula.

Ongezeko la kasi isiyomithilika la watu duniani pamoja na kuongezeka kwa hali bora za maisha                               
vinavyoelekeza ongezeko kubwa la tabaka la kati lenye uwezo mkubwa wa kutumia bidhaa kadha wa kadha na kula chakula kingi zaidi ya watu wa tabaka la chini pamoja na ongezeko la ubora wa huduma za afya na tiba na wingi wa wazee katika;
adhi inayopungua eneo na ubora wake kiuzalishaji
maji yanayopungua kwa kwa kasi na kwa kiasi kikubwa cha kutabiriwa kuwa chanzo au kichochea cha vita vya tatu vya dunia badala ya mafuta kama ilivyodhaniwa awali.
athari za tabianchi duniani kote vikiwemo ukame, majangwa kuongezeka na/au mafuriko kwa upande mwingine.
matumizi yanayobanwa ya mbolea na kemikali mashambani
uhamiaji wa watu mijini na ongezeko la mahitaji ya bidhaa za kilimo kwa chakula na bidhaa nyinginezo hitajifu zitokanazo na mazao ya kilimo.

La nne ni lile linalohusu biashara ya vyakula kuendeshwa kwa uadilifu kuwezesha pande zote kufaidi matokeo ya usambazaji na ulaji.

Na jambo la tano linalozungumzwa ni juu ya uwezo wa Afrika kama kiini na roho ya dunia katika chakula na rasilimali nyinginezo hitajifu za ardhini na majini.

Dunia haiwezi kufanikiwa pasipo mabadiliko Afrika, na hapa itamkwe na ieleweke wazi kwamba pasipo Waafrika wenyewe kufanyiza mabadiliko hayo, wageni watayafanya kwa ujambazi kama walivyokwisha  kutangulia au kwa kurubuni na kuwapiganisha Waafrika wenyewe, wamalizane na wageni kupata nafasi ya kujitwalia watakacho.

China ni mfano mmoja mzuri wa kutuongoza katika kile  kifanyikacho sasa na kutupa mwanga wa kitakachotokea siku za usoni si haba.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya China ya miaka ya karibuni, imeagiza/au itaagiza mchele kwa ajili ya raia wake kutoka nje, jambo ambalo linabadili mwelekeo na mfumo wa uzalishaji na biashara ya vyakula na mazao ya kilimo duniani ikiangaliwa idadi ya Wachina na walivyofanikiwa kuunda tabaka la kati lenye uchu na uwezo wa kula katika siku za karibuni na kwa kasi inayoendelea katika hali ya kasi kubwa ya kupungua kwa ardhi yenye rutuba kwa uzalishaji wa tija(under  plummeting harvestable land per person ratios)

Chakula zaidi kinahitajika kwa watu zaidi, chakula zaidi hata kama si kwa watu zaidi ila kwa watu wanaokula zaidi kwa vile uwezo wao au ukwasi wao unaongezeka kwa kasi na wenye ukwasi  hula zaidi kile watakacho kwa vile ukwasi wao unawawezesha  kupata wakitakacho hata kama ni kwa bei ya kuangamiza wasio nacho au mafukara..

Chakula kwa sasa ndiyo tasnia inayoongoza duniani  kwa utata wake, uhitaji, na  matarajio yasiyoeleweka kwa siku za usoni. Tasnia ya kilimo na chakula inaongoza pia katika matumizi makubwa ya ardhi, matumizi makubwa ya maji, matumizi makubwa ya nishati na kemikali na uchafuzi  mkubwa wa mazingira vyote ambayo  vinahujumu mfumo himilivu wa ekolojia hitajifu duniani.

Mathalani, ongezeko kubwa la watu wenye kipato cha kati hupendelea kula nyama – ambayo ndiyo kipimo cha juu cha uwezo wa familia ingawa kiasi cha 90% cha mazao yatumikayo kulisha mifugo huhitajika kupotea ili, kutengeneza asilimia 10 ya manufaa katika nyama(conversion rate – feed : meat)

Kukua kwa miji na majiji kunazidi kuongeza uhitaji wa uzalishaji mkubwa na wenye tija mashambani  pamoja na athari za matumizi makubwa  na  ya aina lukuki ya vyakula yasiyoendana na uhifadhi na kusababisha upotevu mkubwa(na hapa iunganishwe na upotevu mkubwa wa mavuno ambao hukadiriwa kufikia 60% katika bara la Afrika).

Na kwa vile mazao ya chakula ndiyo yanayofanyiza mzunguko mkubwa wa fedha katika Afrika na ni mhimili wa mahitaji ya viwanda vya kati yumkini kwamba wasomi na wenye maarifa pevu watapoingia katika tasnia hii ndipo Afrika itapoweza kufanyiza mabadiliko makubwa yasiyomithilika katika maendeleo(until the learned go onto agriculture, no changes  can be envisaged in Africa).

Yumkini yote hayo yanaupa mkoa wa Rukwa fursa kubwa katika kilimo kwa rasilmali ardhi,  maji, mwanga, na madini ulivyojaaliwa kiasi cha kuuwezesha kuhimili hali hasi zinazoweza kutokana na hayo kwa miongo kadhaa ijayo kama rasilmali watu itaandaliwa kuvuna na kutumia.

Ikumbukwe kuwa staarabu zote zilizotangulia katika nyayo za mwendo wa binadamu ziliibuka, zilikua zikashamiri, zilianza kufifia na kufa kutokana na kilimo.

ELIMU NA MAARIFA

Umuhimu wa elimu kwa  binadamu  siyo jambo lenye kujadiliwa tena zaidi ya  kuorodheshewa matokeo chanya yatokanayo.

Kukosekana kwa maarifa  ya kutosha katika shughuli nyingi watendazo viongozi na wananchi  katika nchi  maskini  yajadiliwa na kukubalika kwamba  ndiyo kiini cha umaskini  na ukosefu wa maendeleo kwa nchi hizo.

Hata kama nchi imejaaliwa maliasili kwa  kiasi kikubwa  kilioje kama watu wake  hawana maarifa  ya kuwawezesha kuvuna na kutumia maliasili hizo kwa maendeleo yake, nchi  hiyo  haitaweza kupiga  hatua katika  ustawi  wa watu wake zaidi ya kurubuniwa na/au  hata kuibiwa na wageni  wenye maarifa kama ilivyokwisha kuthibitika kwa nchi nyingi za Afrika.

Mkoa wa Rukwa na jirani zake wa  Nyanda za Juu Kusini  ambayo ina uzalishaji mkubwa wa zao la mahindi mathalani,  hawana maarifa  hitajifu kuongeza  thamani  ya mahindi  wazalishayo kuweza kuzalisha  bia katika  Afrika Mashariki na Kati.

Takribani tani laki  nane za mahindi  yatumikayo kuzalisha  bia kwa Tanzania  peke yake huagizwa kutoka nje  ilhali wakulima wa mikoa hiyo  wakikosa soko la mahindi yao na kutopea katika  lindi la  umaskini.

Maarifa  ya kuongeza  thamani  ya mazao  ya kilimo ni kiini cha  ajira, biashara, na ustawi  wa jamii  inayotegemea kilimo katika uchumi wake.

Na bahati  mbaya iliyoje  kwamba wananchi  wenyewe wa mikoa hiyo  hawana  ufahamu wa kuwa hata bia wanywazo hutokana na mahindi.

Chuo kikuu kama  ghala la maarifa,  uwanja wa matumizi ya maarifa, kitovu cha ubunifu na  uthubutu wa  kutenda fikra na kiini cha usambazaji wa maarifa ni  jambo muhali kwa jamii  yoyote  yenye  uhitaji wa maendeleo.

Taaluma  zote na maarifa  ya aina  zote  kwa upeo vyahitajika sana kwa maendeleo  ya wanaRukwa na  Tanzania kwa ujumla.

Maarifa pevu katika  sayansi na teknolojia  hukuza vipaji  vya ubunifu na uthubutu  (creativity and initiatives) zaidi ya matumizi  ya kawaida  ya teknolojia  kutoka kwa wagunduzi  wa  teknolojia  hizo  hata kama mazingira hayafanani.

Uongezaji thamani mazao ya kilimo usipofanyika ni  dhahiri  80%  ya  Watanzania hawatakuwa na uwezo wa  kuondoka  katika lindi  kubwa la umaskini  walimo.

Uongezaji thamani huunda thamani na  ajira pale zilipokuwa zinakosekana.

Na ajira hupata wale wenye ujuzi wa maarifa ya  kutenda kazi zao, na mara  nyingi  watu  wenye  maarifa na ujuzi wa  kutenda  kwa ufanisi ni wale walioelimika kwa maarifa na/au ujuzi.

Walioelimika huweza  kuajiriwa ima  kujiajiri  na  kuunda  ajira na kuajiri watu  wengine na kuwezesha, kukuza na kusambaza vipato kwa watu wengi katika jamii.
Na wenye vipato wana uwezo wa kununua bidhaa iwe za kilimo ima bidhaa lukuki kwa mahitaji  yao ya maisha,  na hivyo  kuwa ni soko zuri kwa bidhaa za ndani na zitokazo nje pia.

Umaskini wa wananchi wa mkoa wa Rukwa ni pamoja na  ule  utakanao na  uwezo  finyu wa kuuza wanachozalisha na hivyo  kuwa na uwezo hafifu wa kununua kwa upande mwingine.

Kuuza alichonacho mtu kwahitaji maarifa ya kuuza, maarifa ambayo  Chuo  Kikuu cha Rukwa kitawajibika kuyajenga, kuyakuza, kuyahimilisha, kuyatafiti  na kuyasambaza kwa wananchi  yapate  kutumika.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia ni kilimo ambacho  kina uwezo wa kubadili maisha kwa kupunguza umaskini kwa kadiri ya mara nne zaidi ya uwezo wa
sekta nyingine yoyote ile duniani kwa sasa.

Aidha kwa taarifa hizohizo za Benki ya Dunia ajira moja katika uchakataji mazao ya kilimo huwezesha uundaji wa ajira tatu hadi nne katika nchi maskini na ajira mbili katika nchi zilizoendelea(multiplier effect).

Mgao wa biashara kisekta duniani unaonyesha kwamba mazao ya kilimo na bidhaa zitokanazo zitachukua nafasi kubwa tangulizi katika muongo mmoja ujao na katika Afrika takriban soko la dola za Marekani trilioni 7 itahusu vinywaji na chakula pekee ifikapo 2014.

Chuo  Kikuu kama  kichocheo  cha mabadiliko na utundu wa  ubunifu, uthubutu (creativity, initiatives) na kama kitovu cha mahusiano na  ushirikiano katika maarifa  na wadau wengine duniani kote;  na kama kituo cha ubadilishanaji maarifa na ujuzi,  tafiti,  uzoefu na  fikra  katika  nyanja  zote  kina wajibu  mkubwa wa matumizi ya maarifa ndani  ya jamii  inayokizunguka.

Na  hayo ndiyo matarajio  ya wanaRukwa kwa Chuo  Kikuu cha Rukwa.

Aina nyingi za mazao  yazalishwayo  mkoani  Rukwa yanatarajiwa kuwezesha  ujenzi wa   viwanda vingi vinavyoweza kutoa ajira kwa kiasi cha kutosheleza mahitaji ya ustawi wa wananchi  wake.

Viwanda vya nafaka na mbegu za mafuta  vinaweza kuzalisha viwanda    vingine kama  vile  vya nyama, ngozi, plastiki (zitokanazo na nafaka na ambazo zinaweza kurejewa matumizi(recycled)  na/au kuozeshwa kuwa mbolea), vifaa vya plastiki hizo, rangi, madawa, wino, vifaa vya ujenzi, vyakula,  vinywaji  karatasi, vilainishi  vya mitambo(castor oil seeds)) viwanda vya mbolea na kualika shughuli za huduma nyinginezo kama mabenki, bima, burudani na sanaa..

Aidha mahala popote duniani kuliko na viwanda vya nafaka ndiko kunakozalishwa mifugo kwa wingi kwa vile nafaka na mabaki(by products) ya michakato ya nafaka zilizoongezwa thamani husindikwa kuwa chakula cha kuku, ngombe, nguruwe na samaki(aquafeed)

Kutokana na mifugo bidhaa za nyama, maziwa na ngozi huzalishwa.

Ngozi nazo zaweza kuzalisha viwanda  vya bidhaa lukuki zitokanavyo  kama vile mabegi, nguo za ngozi, mikanda, mikoba, pochi, vifunikizo(covers) vya samani majumbani na katika vyombo vya usafiri kama magari n .k.

Ikumbukwe pia kwamba kuna bidhaa tele ziwezazo kupatikana katika maziwa kama malighafi
Hata hivyo,  ieleweke kwamba kuendesha viwanda kwahitaji  upeo na viwango vikubwa vya taaluma na maarifa mbalimbali kuweza kuhimilisha(sustain) viwanda hivyo.
Taaluma katika  uzalishaji mashambani (plant agronomy) kwa mfano, ni muhimu ili kuzalisha kwa tija na kwa  wingi mazao ambayo ndiyo malighafi hitajifu  viwandani.
Aidha kwahitajika wanasayansi wa kemia ya udongo(soil chemistry) na maarifa ya mbolea na matumizi yake, na maarifa ya mitambo au mashine za kulimia na  kuvunia, maarifa ya uhifadhi na uendeshaji mitambo ya kuchakata mazao(processing plant machinery operations) kwa viwango vya masoko na ufungashaji(packaging) pamoja na haya kwa uchache;

maarifa katika uuzaji, usambazaji na utafiti masoko.
maarifa katika  utafiti na uongezaji ubora wa bidhaa
maarifa katika sheria mbalimbali za  ardhi, biashara na mikataba.
maarifa katika  utunzaji mahesabu, uhasibu,fedha, na bima za kinga za maisha, biashara na majanga
maarifa katika mienendo ya uchumi na masoko ya fedha
maarifa katika ujenzi miundo-mbinu na  uhandisi  wa umwagiliaji
maarifa katika  sayansi  ya mazingira na tabianchi
maarifa katika misitu, mbao na ufugaji nyuki
maarifa katika utafiti na uzalishaji mbegu
maarifa katika sayansi  ya jamii
maarfa katika ufugaji na tiba ya mifugo
maarifa katika uvuvi na samaki
maarifa katika elimu miamba na madini
maarifa katika uhandisi wa migodi
maarifa katika afya na sayansi ya tiba kwa jamii
Na itoshe kwamba maarifa mbalimbalimbali ambayo kwa pamoja yanategemeza ustawi wa jamii.

Aidha, maamuzi yoyote  yale na popote pale mara nyingi hufanywa  na watu  wenye mawanda mapana katika  fani  husika ili waweze kutoa maamuzi yaliyo bora, yenye dira na mshiko.

Mkoa wa Rukwa waweza kuwa na majaaliwa ya viongozi wazuri sana kwa nafasi zao katika vijiji, ingawa yumkini kukiri kwamba wanapwaya katika upeo wa nafasi zao za uongozi kwa kukosa mawanda mapana ya kuwawezesha kustawisha wananchi wao.
Ni matarajio ya  wanaRukwa  kuwa Chuo Kikuu cha  Rukwa  kitawezesha  upevu wa maarifa lukuki hitajika na  kuwezesha  wana Rukwa kujipatia viongozi wapevu katika ngazi zote ili kuongoza ustawi wa wananchi wao.

Aidha,ni matarajio ya wanaRukwa  kuona Chuo Kikuu ambacho kinatengeneza wahitimu wenye uwezo na ari ya kutumia fursa lukuki zilizopo mkoani kujiajiri na kuunda ajira na kuondokana na dhana ya  kuajirwa hata  pale ambapo wanazo rasilimali zinazoweza kuvunwa na kuwezesha vipato vikubwa na kuajiri watu  wengine.

Chuo Kikuu  Rukwa kinatarajiwa kuzalisha  viongozi wa maendeleo  ya binadamu.

Baadhi ya  bidhaa za viwandani zinazoweza  kuzalishwa kutokana na mazao  ya kilimo katika Mkoa wa Rukwa;

sembe, unga wa ngano, kimea cha shayiri , mchele
vyakula vilivyofungwa katika makopo – maharage, nyanya, samaki  nyama, na matunda(mapapai, maembe, ng’ongo).
vyakula  vya watoto(baby foods).
vyakula vya staftahi(breakfast foods).
     -     vyakula  vya mifugo(feeds).
nyama ya ngombe, kuku, kondoo, mbuzi na mbuni.
mafuta  ya  alizeti, karanga na ufuta
ngozi na bidhaa  zake
mafuta  ya nyonyo(castor oil) na bidhaa zake  lukuki  vikiwemo vilainishi vilivyo bora kuzidi vile vitokanavyo na mafuta madini ya petroli.
gundi  zitokanazo na wanga wa nafaka.
wino  wa printers zitokanazo na wanga wa mahindi.
bia na  pombe kali(whisky, gin) kutokana na sukari za wanga wa mahindi
betri(dry cells) - hutumia unga wa mahindi
sembe kwa ajili  ya sukari ya vinywaji vitamu, madawa na maji ya  kutundikia magonjwa  (corn dextrose for intravenous solutions)
mvinyo wa ming’ong’o (sclerocarya birea) -Amarula
plastiki  zitokanazo na wanga
rangi za majengo na  viundwa mbalimbali
wanga kwa baruti za milipuko mbalimbali(explosives carrier)
sukari  ya  dawa za mswaki
ufugaji wa kuvu (fungus)  aina mbalimbali kwa ajili ya dawa za antibiotic.
chakula cha samaki

No comments:

Post a comment