Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, TAMISEMI, Selemani Jafo, amewataka wasimamizi na wasaidizi wa uchaguzi kote nchini, kuhakikisha wanasimamia zoezi la uchukuaji na Urejeshaji wa fomu kufuata kanuni na sheria zilizowekwa kuondoa dosari zote zilizojitokeza wakati wa zoezi hilo.

Pia amevitaka vyama vya siasa vyote kuhakikisha wanafuata kanuni na sheria pamoja na masharti wakati wote wa zoezi la uchukuaji na Urejeshaji wa fomu za uchaguzi wa serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 mwaka huu.

Waziri Jafo ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya zoezi la uchukuaji fomu ikiwa Leo ni siku ya pili ya zoezi hilo.

Waziri Jafo amesema kiujumla zoezi hilo limeenda vizuri licha ya kuwa na dosari baadhi ya maeneo ambayo yamekumbwa na baadhi ya vikwazo na zoezi hilo likashindwa kufanyika kiufasaha lakini dosari hizo zinafanyiwa kazi.

"Zoezi limeenda vizuri tuna kata 3956 na Kati ya kata hizo ni kata 72 tu ndio zilizokuwa na dosari ambapo zoezi hilo halikufanyika kifasaha na miongoni mwa maeneo yaliyokuwa na malalamiko ni Liwale Lindi, Moshi, Sengerema na Songwe baadhi ya maeneo hayo"

"Niwatake wasimamizi wa uchaguzi na wasaidizi wao katika maeneo yote wahakikishe wanasimamia kwa kuzingatia kanuni na taratibu zote zilizowekwa kuhakikisha wanaondoa changamoto zilizojitokeza wakati wa zoezi hili" amesema Waziri Jafo.

Aidha amesisitiza vyama vyote vya siasa kuhakikisha wanafuata taratibu na kanuni zilizowekwa kwa ajili ya kuepusha uvunjifu wa Sheria na kuvuruga amani wakati wote wa zoezi hilo.

Amesema zoezi hilo ni la siku Saba hivyo Wizara yake ambayo ndio msimamizi wa uchaguzi huo wanaendeleo kuzifanyia kazi dosari zote ambazo zimejitokeza katika maeneo yenye malalamiko wakati wa zoezi hilo kuhakikisha linaisha salama na kila mtu anapata haki yake.

Amesema maeneo yote ambayo zoezi hilo halikwenda vizuri wawasilishe malalamiko yao kwenye kamati za rufaa na maadili zilizopo katika maeneo yao ili kuondolewa kwa dosari ambazo wanahisi hazikuwekwa vizuri wakati wa zoezi hilo.

Aidha amesema maagizo yake aliyoyatoa hayajapuuzwa bali changamoto zilizojitokeza ni za kawaida ambazo hutokea katika uchaguzi wowote duniani na zitaendelea kutatuliwa na Ofisi yake ambayo ndio wasimamizi wa uchaguzi huo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: