WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hajaridhishwa na ujenzi wa kituo cha afya cha Ndago, wilayani Iramba mkoani Singida kwa sababu uko chini ya kiwango.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Oktoba 6, 2019), wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Ndago mara baada ya kukagua majengo ya kituo hicho.

“Nimepita kote nchini kukagua vituo hivi lakini hapa wamenikasirisha. Wamenileta kwenye jengo nilikaguem nikajua ni jipya kumbe ni la zamani. Lazima nikiri kwamba fedha yetu hapa haijakamilika, jengo la mama na mtoto halijakamilika. Nilipouliza linakamilika lini, wananijibu tuko kwenye final touches (tuko hatua za mwisho),” amesema.

“Jengo lile halivutii kabisa, wanaotoa maelezo hakuna kinachoeleweka. Sijaridhishwa kabisa na hali hii. Jengo la upasuaji nalo pia nimeona ni la zamani. Hii ina maana hamjajenga jengo jipya. Mimi nataka nione jengo jipya hapa,” amesisitiza.

Alipomuuliza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw, Leno Mwageni amebakiza kiasi gani cha fedha katika sh. milioni 400 ambazo zililetwa kwa ajili ya ujenzi wa majengo hayo, Mkurugenzi huyo alijibu kwamba hakuna kiasi cha fedha kilichobakia.

Waziri Mkuu aliwaeleza wananchi hao kwamba Mheshimiwa Rais John Magufuli anatambua wao hawana uwezo, na tena wanaugua na kuna watu ambao wanapoteza maisha kwa sababu hawawezi kufika kwenye tiba kwa wakati.

“Vituo vya afya vinajengwa kila mahali nchini ili wewe mwananchi usilipe nauli kwenda Iramba mjini au Singida mjini kutafuta tiba, bali upate vipimo vyote hapa hapa ulipo. Vipimo vya magonjwa yote vinapatikana hapa hapa.”

“Fedha hizi zikiletwa zinataka pajengwe maabara, chumba cha upasuaji mdogo na mkubwa, chumba cha huduma ya mama na mtoto, chumba cha kuhifadhia maiti na nyumba ya mkuu wa kituo, lakini hapa Ndago fedha yetu imeharibika,” amesema.

Alipoenda kukagua chumba cha kuhifadhia maiti, Waziri Mkuu alikuta limewekwa mlango wa mbele tu na vyumba vingine vyote havina milango wala mabomba na masinki hayajakamilika tofauti na taarifa aliyopewa kwamba jengo hilo liko tayari.

“Mkurugenzi nimekuta wagonjwa wamelazwa katika baadhi ya vyumba na kazi haijakamilika. Huwezi kupanga vifaa wakati ujenzi unaoendelea ili kumdanganya Waziri Mkuu. Na wala hunidanganyi mimi bali unawadanganya wananchi.”

“Ninazo taarifa kwamba jana mlikesha kupanga vitu ndani. Nenda kaondoe vifaa vyote hadi ujenzi utakapokamilika ndipo madaktari warudi kuendelea na kazi. Serikali hii haiwezi kuvumilia vitu vya hovyo. Hatua kali zitachukuliwa,” alisisitiza.

Mapema, Mbunge wa jimbo hilo, Bw. Mwigulu Nchemba alimweleza Waziri Mkuu kwamba alichangia mifuko 400 ya saruji na wananchi wa kata hiyo walichangia mawe na ujenzi wa msingi.

Alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Magufuli kwa kuwapatia fedha za ujenzi wa vituo vya afya. “Tunashukuru kwa sababu fedha hizi zimekuja kamili, na siyo kwa mafungu. Wananchi wamechangia nguvu zao na mimi mwenyewe nilitoa mifuko 400 ya saruji,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kumuomba Waziri Mkuu awasaidie wananchi wa kata ya Ndago wapate barabara ya lami ya kutoka Singida-Sepuka-Ndago-Kizaga yenye urefu wa kilometa 76. “Hii ni tarafa kubwa kuliko zote na huku ndiko uzalishaji mkubwa uliko. Hii barabara imeshafanyiwa upembuzi yakinifu, kilio na furaha ya wana-Ndago ni barabara hii kuwekwa lami,” alisema.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Share To:

msumbanews

Post A Comment: