Sunday, 27 October 2019

Makamu wa Rais ataka kuongezwa juhudi zaidi kwa wanawake kuwania nafasi za uongoziHappy Lazaro,Arusha.

Makamu wa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania ,Samia Suluhu  ametaka kuwepo kwa juhudi zaidi kwa ajili ya kuongezeka kwa idadi ya viongozi wanawake  katika  idara  mbalimbali kuanzia  ngazi za  chini hadi juu ili kuendelea kuchochea maendeleo zaidi.

Ameyasema hayo leo wakati akifungua mkutano wa wabunge wanawake kutoka mabunge ya nchi za Afrika wanachama wa jumuiya ya madola unaofanyika jijini Arusha.

Samia  amesema kuwa,kwa sasa hivi kuna  mawaziri wanawake wapatao 7  kati ya mawaziri 23 na manaibu Waziri  wanawake 4 kati ya manaibu 22,hivyo kufanya  wawakilishi wanawake bungeni kufikia asilimia 24.4,hivyo kufanya takwimu hizi kuwa kubwa kuliko nchi zingine.

"pamoja na kuwepo kwa idadi hiyo ya wanawake viongozi bado juhudi zaidi zinatakiwa kuhakikisha kiwango hicho kinaongezeka na kufanya idadi hiyo kuwa juu zaidi  katika ngazi mbalimbali."alisema.

Spika wa bunge la Tanzania ,George Ndugai akizungumza katika mkutano huo,alisema kuwa lengo kuu ni kutaka kuona kunakuwepo kwa uwiano sawa katika nafasi ya uongozi hasa kwa  wanawake bungeni.

Hata hivyo alipongeza  sana kuwepo kwa ongezeko la wanawake viongozi katika mabunge kwani uwepo wao unaleta mchango mkubwa sana na hamasa kwa wanawake wengine kuendelea kujitokeza kwa wingi katika nafasi hizo.

Ndugai aliongeza kuwa, kwa sasa hivi kuna asilimia 30 ya viongozi wanawake kuanzia ngazi ya serikali za vijiji,mitaa,majiji na hata wilaya  ambapo ngazi zote zina wawakili kwa asilimia 30  ,ambapo alitaka juhudi zaidi kuendelea kuongezwa kuhakikisha wanawake wanaongezeka katika ngazi mbalimbali.

Kwa upande wa Mbunge wa Handeni Vijijini , ambaye ni mmoja wa washiriki Mboni Mhita alisema kuwa, dhana kuu ya mkutano huo ni kuangalia nafasi  ya wanawake katika mchakato wa uchaguzi sambamba na kujadili changamoto mbalimbali  wanazokutana nazo katika chaguzi mbalimbali na kuweza kuzipatia muafaka  .

Mhita alisema kuwa,changamto kubwa iliyopo kwa wanawake kushindwa kushiriki nafasi mbalimbali ni kutokana na mfumo dume wa wanawake wengi kuona nafasi hizo ni za wanaume na hivyo wengi wao kujengewa na hofu na kushindwa kushiriki kikamilifu.

"napenda kuwasihi wanawake wote kuhakikisha wanajitoa sana katika kuwania  nafasi mbalimbali za uongozi na kwa wale ambao wameshafanikiwa wahakikishe wanakuwa mabalozi wa kuwainua wanawake wengine."alisema .

Mwisho.


No comments:

Post a Comment