Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Katani Ltd Juma Shamte, akizungumza na mwandishi wa habari ofisini kwake

Na Yusuph Mussa, Tanga


MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Katani Ltd Juma Shamte amesema kusimama kwa viwanda saba vya kusindika mkonge vya kampuni hiyo kumeathiri utendaji, uzalishaji na  kusababisha hasara kama madeni na malimbikizo ya mishahara kwa wafanyakazi na wakulima.


Alisema viwanda saba vya kampuni hiyo vilivyopo kwenye mashamba matano ya mkonge ya Magoma, Magunga, Mwelya, Ngombezi na Hale, vilisimamisha uzalishaji tangu Agosti 21 hadi Desemba 31, mwaka jana baada ya Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela, kutaka Mfumo wa Wakulima wa Mkonge (SISO) kubadili muundo wake ili kuwaingiza wakulima kwenye Vyama vya Ushirika (AMCOS).


Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana Septemba10, 2019 akiwa ofisini kwake jijini Tanga, Shamte alisema madeni hayo kutoka kwa wadau mbalimbali kwa sasa imekuwa ni mzigo, lakini wanajitahidi kuona wanayalipa ili kuweza kuona ufanisi unarudi kwenye viwanda hivyo.


Shamte amelizungumzia hilo baada ya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Kissa Kasongwa kufanya ziara Septemba 2, mwaka huu kwa kutembelea viwanda hivyo ili kuangalia shughuli za maendeleo na kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi. Ni baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi, kuwa bado wanadai mishahara yao.


"Tulisimamishwa na Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) kwa maagizo ya Serikali ya Mkoa kwa matakwa ya kubadilisha mfumo wa Katani Ltd na wakulima. Mfumo kama huu unahitaji maandalizi, lakini tukalazimishwa Januari 2019 tuanze kazi, hivyo kuanza na mfumo huo ambao haupo kibiashara.


"Kusimama na kubadilisha mfumo huo, kumeleta athari na hasara kubwa kwa kampuni, na kuathiri mipango yake kibiashara ya muda mrefu. Pia kumesababisha madeni na kuhatarisha ajira nyingi. Sasa hivi Kampuni inalipa madeni hayo na kufanya Kampuni bado kuwa kwenye hali ngumu ya kibiashara" alisema Shamte.


Shamte alisema ipo haja ya wadau kukaa na kuboresha mfumo wa sasa ili kuweza kuleta tija zaidi kwa wakulima, wafanyakazi na Kampuni ili kuendana na biashara ya mkonge inavyotaka, huku wakulima wakiendelea kulima mkonge, na kuona zao hilo linaendelea kuimarishwa, kwani Kampuni pia ipo kwenye mkakati wa kuongeza Viwanda.


"Tunatarajia mfumo ukiboreshwa na ukawa wa kibiashara zaidi, Kampuni itaendelea kutoa huduma zake kwa wakulima wa mkonge, na ina mpango wa kuongeza viwanda (Korona) ndani ya mkoa wa Tanga, ambapo tunataka kila shamba kati ya mashamba haya matano ya Magunga, Magoma, Hale, Ngombezi na Mwelya kuwa na Viwanda viwili.


"Kinachotakiwa kwa sasa ni makubaliano kati ya kampuni, wadai na wadaiwa wake ili kuwezesha shughuli za kampuni kuwa endelevu wakati mipango ya uwekezaji zaidi inaendelea kukamilika. Nia yetu ni kukifanya kila shamba kuwa na viwanda viwili" alisema Shamte.


MWISHO.
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: