Tuesday, 13 August 2019

Wilaya Ya Kongwa Yapongezwa Kwa Utekelezaji Wa Miradi Ya Kimaendeleo

.
 Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe Deo Ndejembi akizungumza na wananchi wa Wilaya hiyo wakati Mwenge wa Uhuru ulivyofika wilayani hapo kukagua miradi ya kimaendeleo
 Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Ndugu Mzee Mkonge Ally akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma wakati Mwenge wa Uhuru ulivyofika kukagua miradi saba ya kimaendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya hiyo
Sehemu ya wananchi waliojitokeza wakati wa kupokea Mwenge wa Uhuru wilayani Kongwa mkoani Dodoma

Mwenge wa Uhuru umekagua miradi saba ya kimaendeleo wilayani Kongwa mkoani Dodoma na kuipitisha yote huku Mkuu wa Mbio hizo za Mwenge kitaifa, Mzee Mkongea Ally akimpongeza Mkuu wa Wilaya hiyo Mh Deo Ndejembi kwa namna alivyoisimamia na kumtaka kuongeza juhudi zaidi katika kuwatumikia wananchi wake.

Miradi hiyo saba iliyokaguliwa imagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 1.3 ambapo ipo miradi ya Maji, Hospitali, miradi ya Maendeleo ya vijana, Shule ya Sekondari pamoja na kiwanda cha kutengeneza maziwa.

Aidha Kiongozi huyo wa Mwenge alimtaka DC Ndejembi kuwachukulia hatua watumishi ambao wamekua wakikwamisha juhudi za Mhe Rais Magufuli za kuwatumikia Watanzania na kuagiza kuchukuliwa hatua kwa Mhandisi wa Wilaya hiyo, Christian Mlay ambaye aliyedharau ujio wa Mwenge huo.

" Nakuahidi nitamsaka popote alipo mhandisi huyu na nitamchukulia hatua za kinidhamu na kisheria kwa sababu kitendo cha kudharau Mwenge huu wa Uhuru ni kumdharau pia Rais wetu Dk Magufuli, " amesema DC Ndejembi.
Mhandisi huyo Christian Mlay alipaswa kuwepo katika eneo la ujenzi wa madarasa mawili aliyosimamia lakini alipotafutwa hakupokea simu na baadae hakupatikana kabisa. 

Akizungumza kabla ya kuzindua madarasa hayo Mkongea alisema hiyo ni dharau kubwa kwa Rais Dokta John Magufuli na dharau kwa Mwenge uliosisiwa na muasisi wa Taifa hili baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere.

"Nimesikitishwa sana kwa kitendo hiki, mkuu wa wilaya kwa mamlaka uliyonayo hao walioonyesha dharau wachukulie hatua kali ndani ya siku 4 kwa maandishi,

"Nilishatoa taarifa nilipofika tu Dodoma kwamba katika miradi yote tutakayoitembelea ni lazima wawepo wataalam na taarifa ya mradi, sasa hapa mtaalam hayupo wala msaidizi wake,"alisema mkimbiza mwenge huyo.

Akizungumza mara baada ya maelekezo hayo Ndejembi alisema ameyapokea na anayafanyia kazi ili muhusika apatikane mara moja.

Alisema mhandisi Mlay alipaswa pia kuripoti Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) mwishoni mwa wiki yeye na wenzake watatu kwa kosa la kuisababishia hasara serikali kwenye ujenzi wa majengo katika shule ya sekondari ya Kongwa lakini hakufanya hivyo. 

"Wenzie waliripoti Takukuru na kwa afisa upelelezi wilaya wakalala ndani siku moja yeye hakutokea na tangu aliposikia maagizo yangu ndio hajaonekana kabisa, lakini tutamtafuta atapatikana na hatua zitachukuliwa, "aliongeza Ndejembi

No comments:

Post a Comment