Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa akizungumza na Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kijiji cha Magata, wilayani Muleba mkoani Kagera wakati wa ziara ya kikazi yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.



SERIKALI kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imejipanga kikamilifu kuhakikisha inaweka mkakati madhubuti na endelevu wa kuwapata wanufaika stahiki wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na kuwapatia ruzuku zao kwa wakati. 

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa  wakati akizungumza na wananchi na wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Vijiji vya Magata na Kyamyorwa, wilayani Muleba mkoani Kagera ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani humo ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.

Dkt. Mwanjelwa amesema kuanzia sasa wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini watasajiliwa katika mfumo wa kielektroniki ikiwa ni pamoja na kupigwa picha kwa anayesajiliwa na anayesajili wakiwa katika makazi ya mnufaika ili kujiridhisha na sifa za mhusika.

Dkt. Mwanjelwa ameongeza kuwa, katika kuboresha utekelezaji wa Mpango wa TASAF awamu ya tatu sehemu ya pili, wanufaika wa Mpango watapatiwa ruzuku yao kwa njia ya miamala ya simu ili wapate stahiki zao kwa wakati.

“Wanufaika mnatakiwa kuwa na simu za viganjani zitakazowawezesha kupokea ruzuku zenu halisi na kwa wakati,” Dkt. Mwanjelwa amesema.

Dkt. Mwanjelwa amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kuwajali wanyonge hivyo, itahakikisha kila mnufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini anapata stahiki yake.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: