Monday, 12 August 2019

Waliofariki ajali ya lori la mafuta yafikia 75

Idadi ya watu waliopoteza maisha kwenye ajali ya moto iliyotokea juzi Jumamosi Agosti 10, 2019 mkoani Morogoro nchini Tanzania imefika 75.

Idadi hiyo imeongezeka baada ya wengine wanne kufariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam walikohamishiwa kwa matibabu zaidi.

Hospitali hiyo ilipokea majeruhi 46 kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya matibabu zaidi hata hivyo, saba kati yao wamefariki.

Akizungumza leo Jumatatu Agosti 12, 2019 Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano MNH Aminiel Aligaesha amesema kwa sasa idadi ya majeruhi wanaoendelea kupatiwa matibabu ni 39.

“Tumepoteza wenzetu wengine wanne na miili yao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti hivyo kama kuna ndugu wa karibu waje kwa ajili ya kuwatambua ndugu zao,” amesema Aligaesha.

Kuhusu hali za majeruhi mkuu huyo wa kitengo cha mawasiliano amesema wanaendelea vizuri na wapo wanaoonyesha matumaini.

No comments:

Post a Comment