Monday, 5 August 2019

Vijana zaidi ya 2000 Manyara washiriki sherehe za KimilaNa Ferdinand Shayo, Manyara

Vijana wa jamii ya Wamasai zaidi ya vijana 2000 katika kijiji cha Irkujit  kata ya Edonyongijape Wilaya ya Simanjiiro mkoani Manyara wameingia kwenye rika jipya linalojulikana kama Irkimayan  ikiwa ni miaka 10 baada ya kumaliza jando.


Kiongozi wa Mila wa rika hilo maarufu kama Laigwanan Lembris Moringe alisema hao kwa sasa wanafurahi kuingia kwenye rika jipya ambapo wataendeleza ushiriki wao katika masuala ya kijamii na kuchangia maendeleo.


Lembris amesema kuwa  vijana wengi hawamiliki ardhi hivyo ameiomba serikali za vijiji kuweka utaratibu wa kutoa maeneo kwa ajili ya vijana ili waweze kushiriki katika shughuli za kijamii na kiuchumi kwa kutumia ardhi kama nyenzo muhimu.

Lembris aliwataka vijana kujitokeza katika masuala ya kijamii na kuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto zilizoko kwenye jamii pamoja na kuchangia katika shughuli za maendeleo.

Diwani wa kata ya Endonyongijape Lucas Moringe ameuagiza uongozi wa vijiji vyote katika kata hiyo kuweka vikao na kutenga maeneo kwa ajili ya vijana ili waweze kujiletea maendeleo yao kwa kutumia ardhi kwa ajili ya kilimo,ufugaji na biashara.

Moringe alisema kuwa serikali itaendelea kuwa bega kwa bega na vijana na kuwawezesha kupitia mikopo ya asilimia 10%  kwa wanawake na vijana ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya alisema kuwa vijana ndio msingi wa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla hivyo wanapaswa kupewa kipaumbele na kushirikishwa katika shughuli za kimaendeleo.

"Katika kata hii kuna kero ila tunashuru serikali  tayari imetenga kiasi cha shilingi bilioni 41.3 za kuvuta maji kutoka mto Ruvu  jitengeni mradi ambao utamaliza kero ya maji katika kijiji hicho na wilaya ya Simanjiro kwa ujumla,” alisema Mbunge huyo.

No comments:

Post a Comment