Na. Paschal Dotto-MAELEZO
Tanzania imepiga hatua kubwa katika masuala ya usawa wa kijinsia kwa yake miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za kusini mwa Afrika (SADC) kwa kuwawezesha wanawake kuweza kujikita zaidi katika kujiwezesha kukuza mitaji na kuinua uchumi wao.

Akizungumza katika uzinduzi wa Machapisho ya kuimarisha usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake kwa Nchi za Kusini mwa Afrika, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe.Ummy Mwalimu, alisema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kutambua sheria za usawa wa kijinsia kwani baadhi ya masuala ya kuwawezesha wanawake  katika sekta mbalimbali yanaonekana.

Waziri Ummy aliyataja machapisho  hayo kuwa ni chapisho la Mkakati wa SADC kuhusu wanawake, Amani na Usalama, ufuatiliaji kuhusu masuala ya Jinsia na Maendeleo, Mkakati wa SADC kwa ajili ya kushughulikia ukatili wa kijinsia, Ufuatiliaji wa SADC kuhusu sekta ya nishati na Mpango-kazi wa SADC katika suala la Maendeleo yote yakilenga kuwawezesha wanawake wa Jumuiya ya Kusini mwa Afrika.

“Serikali ya Tanzania inatambua uwepo wa usawa wa kijinsia pamoja na uendelezwaji wanawake katika nchi yetu, na hili limetambuliwa katika Katiba yetu kama suala muhimu kwa haki za binadamu, na lipo kwenyedira ya maendeleo ya 2025 ambapo wanawake wamehusishwa zaidi katika kuifikisha Tanzania uchumi wa kati”, Waziri Ummy.

Waziri alisema kuwa mwaka 2000 Serikali iliweka sera kuhusu masuala ya wanawake na maendeleo ya kijinsia nchini, ambapo katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kifungu namba 66(1) kinachoeleza ushiriki wa wanawake katika masuala ya bunge kwa Asilimia 30.

Katika kutekeleza hilo, Serikali iliweka viti maalum kwa wabunge wanawake, na mpaka sasa ubunge kwa wanawake viti vimeongezeka kutoka asilimia 22 mwaka 2005 mpaka asilimia 37 mwaka 2019, na. kwa kuzingatia zaidi, nchi imeweza kuweka historia kwa Nchi za Kusini mwa Afrika kwa kuwa na Makamu wa Rais mwanamke (Samia Suluhu Hassan).

Waziri Ummy alisema idadi ya majaji imeongezeka kutoka asilimia 34 mwaka 2005 mpaka asilimia 41 mwaka 2019, akaongeza kuwa kwa sasa Tanzania inatekeleza mpango wa kuwainua wanawake wajasiriamali kwa kuwapa mikopo nafuu kwa shughuli zao za ujasiriamali.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt.Stagomena Tax alisema kuwa Serikali ya Tanzania inafanya vizuri katika kuweka usawa kwa jinsia zote, akaeleza kuwa katika tathmini, sera za kikanda na kitaifa zimehuishwa lakini  bado ukanda huo wa Afrika haujafikia malengo ya kuwa asilimia 50 kwa 50 hasa katika masuala ya siasa.

Dkt.Stagomena alisema katika ukanda huo wa Afrika nchi zinazofanya vizuri kwenye masuala ya siasa kwa kuweka 50 kwa 50 ni pamoja naAfrika Kusini na Visiwa vya Ushelisheli, lakini kwa nchi ambazo zinakuja vizuri kwa sasa ni Tanzania.

“Ukiongelea Usawa wa Kijinsia kwenye siasa ni maana ya 50 kwa 50, katika ukanda wetu wa Kusini mwa Afrika, nchi ambazo zimefikia hatua hiyo ni Afrika ya Kusini na Sheliseli, lakini Tanzania ipo kwenye nafasi nzuri kwa nchi ambazo ziko juu”, Dkt.Stagomena Tax.

Aidha, Dkt. Stagomena alieleza kuhusu masuala ya nishati na kueleza jinsi Tanzania inavyokuja kutatua masuala nishati kwa kujenga mradi mkubwa wa umeme Julius Nyerere Hydro Power Project(JN HPP), na mkakati mkubwa kwa SADC ni kuweza kuzalisha na kuleta umeme pamoja “kwenye power pool”, kwa hiyo mradi huo utasaidia ukanda huo wa Afrika.

Naye, Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani, alieleza jinsi Tanzania inavyojikita katika kutekeleza mipango mikakati ya kufikia Megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025, ambapo Tanzania itaweza kuchangia umeme mkubwa kwenye “Power pool” ya nchi za SADC na kuweza kuimarisha upatikanaji wa umeme ukanda huo wa Afrika.

“Mkakati mkubwa wa SADC ni kuimarisha miundombinu ambayo inachochea ukuaji wa uchumi wa viwanda, na nchi wanachama tumekubaliana mambo makubwa manne ambayo ni kuzalisha umeme wa kutosha kama nchi, kujihakikishia umeme unaotabirika, na kuchangia umeme katika mradi wa pamoja unaoitwa (SADC Power Pool)”, Alisema Dkt.Medard Kalemani.

Alisema kuwa Tanzania ina vyanzo vingi vya kuzalisha umeme ikiwemo gesi ambayo kwa sasa inazalisha kiasi cha Megawati 884, lakini Serikali inafanya jitihada za kuvumbua gesi asilia ambayo ipo takribani futi za ujazo trilioni 57.54 na kati ya hiyo trilioni 8.8 inatumika kuzalishia umeme kwa sasa.

Alisema kuwa masuala ya kuwa na umeme mwingi kwa Nchi za Kusini mwa Afrika kutasaidia wanawake wengi kutotumia nishati mbadala kama vile kuni inayotokana na ukataji miti, kwa hiyo machapisho hayo yamekuja muda muafaka wa kufanya mapinduzi ya nishati kwa Nchi za SADC.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: