Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kulia),akimkabidhi Cheti Mtumishi wa Wizara hiyo kutoka Tanzania Bara, Bi. Patricia Mlowe,wakati wa hafla ya kuagwa rasmi kwa ajili ya safari ya kwenda masomoni Uingerezakwa udhamini wa Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID), hafla iliyofanyika jijini Dares Salaam, wa pili kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Amina Shaaban.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kulia),akimkabidhi Cheti Mtumishi wa Wizara hiyo kutoka Zanzibar, Bw. Hamad Said, wakati wa hafla ya kuagwa rasmi kwa ajili ya safari ya kwenda masomoni Uingereza kwa udhamini wa Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID), hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam, wa pili kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Amina Shaaban.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia), akimpongeza mtumishi wa Wizara hiyo, Bi. Diana Ulomi, aliyepata fursa ya udhamini wa masomo katika vyuo vikuu nchini Uingereza kwa kiwango cha Shahada ya Uzamili uliotolewa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Uingereza (DFID)
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa nne kulia), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi Amina Shaaban (wa tatu kushoto) Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID), Bi. Beth Arthy (wa tatu kulia) na wajumbe wengine kutoka Tanzania na British Council-Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja wa watumishi waliopata fursa ya kwenda kusoma Uingereza kwa udhamini wa DFID.

**************

Na. Peter Haule, WFM, Dar es Salaam

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amewataka Watumishi wa Wizara hiyo waliopatiwa ufadhili wa masomo na Serikali ya Uingereza kupitia Shirika lake la Maendeleo (DFID) katika vyuo vikuu vya nchi hiyo kusoma kwa bidii ili kuja kulitumikia taifa kwa umahili zaidi katika nyanja za uchumi na uchambuzi wa masuala ya fedha.

Hayo yameelezwa na Waziri huyo wakati wa hafla ya kuwaaga rasmi watumishi watano wa Wizara hiyo waliopata udhamini huo, iliyofanyika katika Ofisi za British Council- Tanzania, jijini Dar es Salaam.

Dkt. Mpango alisema kuwa, miaka miwili iliyopita aliiomba Serikali ya Uingereza kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Uingereza (DFID), wasaidie kusomesha watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango kwenye Vyuo vikuu vya Uingereza, kwa kuwa Wizara ya Fedha katika nchi yeyote ndio nguvu ya fikra katika Serikali, hivyo bila watumishi wenye ujuzi kutakua na wizara dhaifu.

“Ninawasisitiza sana vijana waliopata fursa ya kwenda kusoma Uingereza, wajue dhamana wanayokwenda nayo, watanzania takribani milioni 50 wanaimani nao, wanamatarajio kwamba watakapokwenda huko watazingatia kusoma kwa bidii, ili wakirudi wawe wataalam waliobobea katika masuala ya uchumi na uchambuzi wa masuala yote ya fedha ndani ya Wizara”, alieleza Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango alisema kuwa, pamoja na kuiomba Serikali ya Uingereza kutoa mafunzo kwa vijana hao aliwaomba pia iwapatie mafunzo kwa vitendo katika taasisi zinazojihusisha na masuala ya uchumi na fedha nchini humo ili wapate udhoefu.

Alisema anaishukuru Serikali ya Uingereza kwa kukubali ombi hilo na sasa ni timu ya tatu kupelekwa masomoni, awamu ya kwanza na ya pili walipelekwa jumla ya vijana kumi, na sasa tumewaaga rasmi watumishi watano ambao wataenda mwezi ujao na kufikisha idadi ya watumishi 15.

Amewataka watumishi hao wakaitangaze vizuri Tanzania na wakirudi waje kuitumikia Tanzania ili taifa lipate maendeleo yanayotarajiwa baada ya hatua hiyo muhimu ya kuwekeza kwa vijana watanzania katika kupata ujuzi.

Kwa upande wake Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa Uingereza (DFID), Bi Beth Arthy, alisema kuwa tangu mpango huo uanze Serikali yake imekwisha wasomesha wanafunzi kumi katika fani za uchumi na uchambuzi wa masuala ya fedha na idadi ya watumishi watano watakao kwenda kusoma nchini humo itafikisha idadi ya watumishi 15.

Alisema kuwa lengo la hatua hiyo ni kuisaidia Serikali kuimarisha utawala wa fedha, masuala ya usimamizi wa kodi na mifumo ya kifedha.

Aidha amewapongeza waliofanikiwa kufuzu mitihani mbalimbali iliyowawezesha kupata nafasi hizo kwa watumishi wa Wizara hiyo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na kuwataka kufanya bidii kwa kuzingatia masomo ili watakapomaliza masomo yao warudi kulitumikia Taifa la Tanzania.

Watumishi waliopata ufadhili wa masomo kupitia Shirika la DFID ni pamoja na Patricia Mlowe, Diana Ulomi, Alex Mwakisu, Martha Luanda na Hamad Bakar Said.

Kwa upande wa wanufaika kupitia wawakilishi wao, Bi. Diana Ulomi na Hamad Said waliishukuru Serikali ya Uingereza na Wizara ya Fedha na Mipango kwa jitihada za kufanikisha kuwapatia masomo kwa ngazi ya Uzamili ili kuongeza ujuzi wa kulitumikia taifa katika masuala ya uchumi hasa kipindi hiki ambacho Tanzania inaelekea katika uchumi wa kati uliojikita katika Viwanda na wameahidi kusoma kwa bidii ili kufikia malengo hayo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: