Tuesday, 13 August 2019

TAMISEMI YAOKOA BILIONI 1.2 UJENZI WA HOSPITALI MOROGORO.Na. Angela Msimbira  - Malinyi, Morogoro.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  Selemani Jafo ameiagiza timu ya wataalam wa ufuatiliaji wa fedha za miradi kutoka OR-TAMISEMI kufanya uchunguzi wa matumizi ya shilingi bilioni 1.2 zilizotumika kwaajili ya ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa Hospitali yaWilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro.

Ametoa maagizo hayo leo wakati akiongea na wananchi wa Halmashauri hiyo kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Halmashauri yaWilaya ya Malinyi, Mkoani Morogoro.

Amesema kuwa wataalam hao watakwenda kufanya uchunguzi wa kina na ufuatiliaji wa ununuzi wa  vifaa vya ujenzi uliofanyika katika Ujenzi wa Hospitali hiyo lengo likiwa ni kuhakikisha matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali yanaendana na majengo yaliyo jengwa.

Amesema kuwa endapo itabainika kwamba kunamakosa yalifanyika hatua zitachukuliwa lakini baada ya kujirizisha kwa kuwa taarifa ya awali inaonyesha fedha hizo zimeliwa na Ofisi yaHalmashauri ya Wilaya ya Malinyi.

“Taarifa ya awali inaonyesha kuwa shilingi bilioni 1.2 zilizotumika kwaajili ya ununuzi wa vifaa vya Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Malinyi hazikufuata taratibu, ndio maana OR-TAMISEMI inakuja kujiridhisha zaidi kabla ya kuchukua hatua” Anasisitiza Jafo.

Wakati huohuo  Jafo amesema kuwa hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa Hospitali hiyo na ametoa mwezi mmoja kwa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanamaliza ujenzi kwa asilimia 100.
 

“Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi sijarizishwa na kasi ya ujenzi wa hospitali hii hakikisheni mnafanyakazi usiku na mchana ili ifikapo tarehe 30/9/2019 ujenzi uwe umekamilika” Anasisitiza Jafo.

Ameendelea kufafanua kuwa pamoja na maelezo aliyopatiwa na Mkuu wa Wilaya ya Malinyi na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo bado wameshindwa kukamilisha ujenzi wa Hospitali hiyo kwa wakati jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo katika Halmashauri hiyo.

Amesema kuwa utaratibu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwasasa ni kuwatoa viongozi na watumishi wote ambao wanashindwa kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yao na kukwamisha juhudi za Serikali za kuleta maendeleo kwa jamii.

Jafo ameendelea kusema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi ni eneo ambalo limejaa makundi jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo na kukwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri hiyo hivyo amewataka viongozi kushirikiana na kuleta mabadiliko.

Amesema kuwa inasikitisha kuona kwamba katika utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya afya Mkoa wa Morogoro bado nitatizo ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi jambo ambalo halileti picha nzuri kwa jamii.

Jafo ameuagiza Uongozi wa Halmashauri hiyo kufanya kazi kama timu na kuacha tofauti zao ili kuleta maendeleo katika Halmashauri hiyo.

Aidha, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Mussa Mnyeti amemuhakikishia Jafo kuwa shilingi bilio ni 1.2 zimetumika kwenye manunuzi ya vifaa vya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Malinyi na kumuhakikishia kuwa vifaa hivyo tayari vimesha nunuli wa kwaajili ya kukamilisha ujenzi huo.

No comments:

Post a Comment