Rais Dkt. John Magufuli ametangaza siku 3 za Maombolezo ya Kitaifa kuanzia jana Jumamosi tarehe 10 Agosti, 2019 kufuatia vifo vya watu zaidi ya 60 vilivyosababishwa na ajali ya kuungua kwa moto wakati wakichota mafuta yaliyokuwa yakimwagika baada ya lori la mafuta kupinduka Mjini Morogoro.

Ajali hiyo imetokea jana majira ya saa 2 asubuhi ambapo lori lenye shehena ya mafuta ya petrol limepinduka jirani na Kituo Kikuu cha Mabasi cha Msamvu Mjini Morogoro wakati dereva alipokuwa akijaribu kumkwepa mwendesha pikipiki.
Pamoja na zaidi ya watu 60 kufariki dunia watu wengine takribani 70 wamejeruhiwa na wanapatiwa matibabu katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro na Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli amemtuma Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kumwakilisha katika mazishi ya Marehemu wa ajali hiyo yanayotarajiwa kuanza leo Jumapili tarehe 11 Agosti, 2019.
Katika kipindi cha maombolezo bendera zote zitapeperushwa nusu mlingoti.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: