Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Morris Limbe kumlipa fedha Mkandarasi anayekarabati shule ya sekondari Bukoba ili aweze kuendelea na kazi na kukamilisha ukarabati huo kwa wakati

Naibu Waziri Ole Nasha ametoa agizo hilo mkoani Kagera wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo ya sekta ya elimu inayotekelezwa mkoani humo, ambapo amesema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilishapeleka fedha zote za ukarabati huo kiasi cha shilingi bilioni 1.4 lakini mpaka sasa mkandarasi huyu amelipwa kiasi cha shilingi milioni 32 tu.

“Fedha zilishaletwa zote na wizara shilingi bilioni 1.4 lakini mpaka sasa Mzinga wamelipwa shilingi milioni 32 tu kati ya milioni mia mbili na zaidi walizotakiwa kuwa wamelipwa mpaka sasa, hivyo Mkurugenzi wa manispaa dirisha likifunguliwa hakikisha Mzinga wanapata fedha ambazo wanadai” amesisitiza Ole Nasha.

Ole Nasha amesema ukarabati wa shule hiyo unaoendelea umechelewa kukamilika kwani licha ya fedha hizo kupelekwa mapema mkandarasi amechelewa kuanza kufanya ukarabati huo. Hata hivyo amesema kasi ya ujenzi huo si mbaya kutokana na kuanza mwezi wa tano.

Aidha, Ole Nasha amewataka watendaji wa manispaa hiyo kufuatilia kwa ukaribu matumizi ya fedha hizo kwani ni nyingi kutumika kwa ukarabati ukilinganisha na fedha zinazotumika katika miradi mingine, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa fedha kubaki na kutumika katika kufanya shughuli nyingine za kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

“Nikifananisha fedha ambazo tumetumia kwenye maeneo mengine na miradi mingine mfano miradi ya afya ambao wanatumia bilioni 1.5 kujenga hospitali kubwa kwa kujenga majengo mapya makubwa saba lakini sisi hiyo bilioni 1.4 ambayo inakaribiana na bilioni 1.5 ya afya tunakarabati majengo tu, kuna umuhimu wa kuzisimamia fedha hizi kwa ukaribu," alisema Ole Nasha.

Aidha, Naibu Waziri amesema shule hiyo ina nafasi finyu ikilinganishwa na idadi kubwa ya wanafunzi mia saba waliopo na  amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo kuwasiliana na Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) ambao wana eneo karibu na shule hiyo washaurine juu ya uwezekano wa  kutoa eneo hilo kwa ajili ya upanuzi wa shule hiyo.

Awali Mkuu wa shule ya Sekondari Bukoba, Raymond Mutakyawa, amemweleza Naibu Waziri kuwa ukarabati wa shule hiyo ulikuwa ufanyike kwa siku sabini tano na ulipaswa kuwa umekamilika mwishoni mwa mwezi wa saba lakini ulisimama kutokana na kukosa fedha za kununua vifaa kwa ajili ya kazi hiyo baada ya mfumo wa malipo kufungwa kabla ya fedha hizo kulipwa kwa mkandarasi.

Shule ya Sekondari ya Bukoba inafanyiwa ukarabati na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia baada ya kuharibiwa na tetemeko la ardhi la mwaka 2016 lililoikumba mkoa wa Kagera ambapo baadhi ya kuta za shule hiyo zilianguka na majengo mengine kupata nyufa na baadae paa kuezuliwa na upepo mkali.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
05/08/2019
Share To:

msumbanews

Post A Comment: