Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, amelitaka Jeshi la Polisi kuwakamata wanaosambaza picha za marehemu mitandaoni.

Masauni alitoa kauli hiyo jana mjini Morogoro mara baada ya swala ya Eid iliyofanyika katika Msikiti Mkuu wa Mkoa huo.

Kiongozi huyo wa wizara alisema kusambaza mitandaoni picha za marehemu ni kuwadhalilisha wahusika na ni uvunjaji wa sheria za nchi.

"Ninaziagiza mamlaka na vyombo vinavyohusika vihakikishe vinafuatilia na kuchukua hatua kwa wale ambao wanakiuka sheria za nchi yetu kwa kusambaza mitandaoni picha za marehemu," aliagiza.

Masauni alisema siyo vema kuanza kutumia majanga ya kitaifa kama lililotokea Morogoro la watu zaidi ya 70 kufariki dunia ndani ya muda mfupi, kuanza kusambaza picha za waathirika mitandaoni kwa dhamira ya kudhalilisha.

"Watu hawa wamefariki dunia na mtu yeyote katika tukio lile angekufa, mimi au wewe, ndugu yako au jamaa yako, fikiria kama ni jambo limekukuta au ndugu yako halafu ukachukua picha na kuisambaza kwenye mitandao, katika mazingira kama yale," Masauni alisema.

Alisema  kufanya hivyo siyo tu kunavunja sheria za nchi, bali pia ni kinyume cha utamaduni wa Mtanzania.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: