Mahakama Kuu ya Tanzania imetupilia mbali mapingamizi ya  Serikali kupinga kusikilizwa kwa maombi ya kesi namba 18/2019 ya Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu kuhusu ubunge wake kwa sababu hazina mashiko.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu Agosti 26,2019 na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Jaji Sirillius Matupa wakati akitoa  uamuzi wa pingamizi la awali dhidi ya maombi ya Lissu lililowekwa na Serikali katika maombi yake ya kibali cha kufungua shauri ili kupigania ubunge wake. 

Jaji Matupa ametupilia mbali hoja za pingamizi la awali la Serikali isipokuwa hoja moja tu ya kasoro katika viapo vinavyounga mkono maombi ya Lissu.

Kutokana na kasoro hizo Jaji Matupa amesema inapotokea kuwa kuna aya zenye kasoro za kisheria namna pekee ni kuziondoa aya hizo katika kiapo hicho na kuangalia kama aya zinazobaki zinaweza kusimama na kuthibitisha maombi.

“Nikiangalia hapa aya zinazobaki hapa baada ya kuziondoa hizo zenye kasoro, ninaridhika kabisa kuwa zinaweza kuthibitisha maombi.”, amesema Jaji Matupa na kuongeza:

"Hivyo hoja zote za pingamizi la Serikali zimekataliwa isipokuwa hizo zenye upungufu kwenye hati za viapo. Ukiachilia mbali kasoro hizo za viapo, mambo mengine yote yataasikilizwa wakati wa usikilizwaji wa maombi ya msingi.”
Share To:

msumbanews

Post A Comment: