Mkuu Wilaya ya Arumeru Jerry Muro, amewataka madiwani wa Halmashauri ya Arusha, kufanya uongozi wa kimkakati kwa kujikita zaidi, kuhamasiaha wananchi wao, kishiriki kwa hali na mali shughuli za kimaendeleo na kuacha kusubiri kuihoji serikali kuwaletea maendeleo katika maeneo yao.
Akizungumza na madiwani hao, katika mkutano wa Baraza la Madiwani wa kujadili taarifa za robo ya nne na ya mwisho, kwa mwaka wa fedhe 2018/19, mkutano uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo, amesema maendeleo ya nchi yoyote duniani huanzia kwa wananchi wenyewe, hivyo hamna budi kuwahamasisha wananchi wenu,  katika suala zima la kujiletea maendeleo yao.
Amefafanua kuwa, uongozi wa kimkakati ni kukaa na wananchi wako, kuweka mipango thabiti ya maendeleo katika maeneo yenu, na kuwashawishi kuanza kuitekeleza kwa kuanza kwa nguvu zao wenyewe na sio kiongozi kusubiri vikao vya halmashauri, kuhoji serikali italeta lini fedha kwa ajili ya maendeleo yenu wenyewe.
"Uongozi ni namna ya kushawishi wananchi kushiriki katika kujiletea maendeleo, na sio kazi ya kusimama na kuwatetea tu kwenye vikao, na kuisubiri serikali kuwafanyia kila kitu, imefika wakati, kiongozi kutumia nafasi yako, kuwashawishi wananchi wako kishiriki kuchangia maendeleo kwenye maeneo yenu, vinginevyo mtasubiri sana" amesema Mkuu huyo wa wilaya.
Muro amewataka madiwani hao, kuiga mfano wa madiwani wa Halmashauri ya pacha ya Meru, ambapo wao hutumia nguvu kubwa katika kuhamasisha wananchi kushiriki katika, shughuli za maendeleo na kwa kushirikisha wadau mbalimbali kutekeleza miradi katika sekta zote za Elimu, Afya, Maji na hata kukarabati miundombinu barabara za ndani wenyewe.
Akititolea mfano halisi, Mkuu huyo wa Wilaya amesema, Madiwani wa halmashauri ya Meru baada ya kuona barabara zao zimeharibika, madiwani wameamua kushirikisha wananchi na wadau wa maendeleo kuanza kuzifanyia ukarabati bila kusubiri TARURA, ambapo kwasasa shughuli za ukarabati zinaendelea katika maeneo mbalimbali ndani ya halmashauri ya Meru.
"Mkisema ninyi viongozi mnasubiri TARURA kutengeneza barabara za mitaani kwenu, mnajidanganya na kuwadanganya wananchi waliowachagua, bila kubadilika na kuchukua hatua,  nasema mtasubiri mpaka mwisho wa dahari, na muda wenu wa uongozi utakwisha na hamtarudi" amesema Muro
Aidha amewataka madiwani hao, kuacha kukodisha mitambo ya halmashauri, na badala yake kujipanga kutumia mitambo hiyo, kukarabati barabara katika maeneo yao, kwa kuwahamasisha wananchi kuchangia, pamoja na kutafuta fedha kwa  wadau wengine wa maendeleo kufanya shughuli hizo.
Hata hivyo, ameupongeza uongozi wa halmashauri hiyo pamoja na watalamu wote, kwa kutekeleza shughuli mbalimbali kisekta kwa mwaka wa fedha uliomalizika, hasa kwa kujikita kwenye maslahi ya wananchi, na zaidi katika sekta ya elimu, ambapo Januari mwaka huu wameanzisha shule mbili za sekondari, na wanatarajia kusajili shule nyingine tatu za sekondari  Likamba, Losinoni Juu na Kiserian, ambazo zinatarajiwa kupokea wanafunzi ifikapo Januari 2020 na kusisitiza kujipanga vema kuhakikisha kila tarafa inakuwa na shule ya sekondari kwa kidato cha tano na sita.
Aidha amewahakikishia waheshimiwa madiwani kuwa serikali ya awamu ya tano itaendelea kutoa ushirikiano katika kutekeleza shughuli za maendeleo kwa maeneo yote bila ya kujali itikadi za vyama vyao na kuwataka kujipanga upya kwa mwaka huu mpya wa fedha 2019/19 kuleta mabadliko ya kasi katika maeneo yao.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: