Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Tanzania Ndg Andy Karas katika Ofisi za Wizara ya Kilimo Jijini Dar es salaam, leo Tarehe 1 Julai 2019. (Picha Zote Na Mathias Cnal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa na picha ya pamoja na mratibu wa mradi wa maboresho ya sera (ASPIRES) Prof David Nyange katika Ofisi za Wizara ya Kilimo Jijini Dar es salaam, leo Tarehe 1 Julai 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Tanzania Ndg Andy Karas katika Ofisi za Wizara ya Kilimo Jijini Dar es salaam, leo Tarehe 1 Julai 2019. Wengine pichani ni Naibu Mkurugenzi wa ofisi ya ukuaji wa uchumi (USAID) Tanzania Bi Michelle Corzine, na Mtaalamu wa sera katika usimamizi wa miradi Ndg Semaly kisamo

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo - Dar es salaam

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) leo Tarehe 1 Julai 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAIDNdg Andy Karas katika Ofisi za Wizara ya Kilimo Jijini Dar es salaam.

Katika mazungumzo hayo Mhe Hasunga amemueleza Mkurugenzi huyo kuwa Wizara ya Kilimo imejipanga kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo ili kuondokana na dhana ya kilimo cha kujikimu na kuhamia katika kilimo cha kibiashara. Waziri Hasunga alisema kuwa ili kuongeza tija katika Kilimo, Wizara yake imejipanga kuimarisha utafiti.

Alisema kuwa maendeleo ya kilimo yanategemea zaidi utafiti hususani wa udongo vilevile kubaini teknolojia bora itakayo pelekea kukisogeza kilimo katika hatua kubwa ya mafanikio na kimageuzi.

Amesema kuwa pamoja na mambo mengine wizara ya kilimo pia imejipanga katika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kuliko kusafirisha pasina kuongeza thamani.

“Tukiongeza thamani ni wazi kuwa uchumi utapanda, lakini zaidi ajira ziataongezeka kwa wananchi, tutakuwa na Pato zuri la kigeni sambamba na utambulisho wa nchi” Alikaririwa Mhe Hasunga

Kuhusu sekta ya umwagiliaji Mhe Hasunga alisema kuwa Tanzania ina jumla ya Hekta zaidi ya Milioni 29 zinazofaa katika umwagiliaji lakini ni hekta 475,000 ndizo ambazo zimefanyiwa kazi.

“Kwa maana hiyo kuna fursa kubwa katika umwagiliaji hivyo ninyi kama wadau kadhalika natoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kuwekeza katika umwagiliaji” Alisema

Kuhusu Lishe Waziri Hasunga alisema kuwa wizara imeendelea kuweka hamasa kwa wakulima ili kuwa na lishe bora. Aliongeza kuwa watanzania wanapaswa kuwa na utamaduni wa kula vizuri ili kuondokana na magonjwa mbalimbali kama vile utapiamlo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAIDNdg Andy Karas ameipongeza serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli kwa mikakati madhubuti ya kuimarisha sekta ya kilimo nchini.

Aidha, Karas amemuomba Waziri wa Kilimo kuteua watu wawili kutoka wizarani watakaokuwa kiungo muhimu baina ya serikali na miradi ya USAID sambamba na mtu atakayeratibu mikutano ya wadau wa maendeleo.

MWISHO


Share To:

Post A Comment: