15 Julai, 2019
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
MAPAMBANO
YA RUSHWA YANG’ARISHA OFISI YA RAIS NA OFISI YA WAZIRI MKUU
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema juhudi za Serikali za kupambana na rushwa, kudhibiti
upotevu wa mapato, matumizi ya fedha za Serikali na kusimamia uwajibikaji kwa
watumishi wa umma ni sababu zilizowezesha Ofisi ya Rais pamoja na Ofisi ya
Waziri kuaminika zaidi.
Ameyasema
hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na viongozi wa Umoja wa Wanake
Tanzania (UWT) akiwa katika ziara yake
ya kikazi mkoani Kigoma. Amesisitiza kuwa vita dhidi ya rushwa ni endelevu.
Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais
Dkt. John Magufuli imepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya rushwa ambapo kwa
Afrika Tanzania inaongoza kwa mujibu wa ripoti ya taasisi ya Transparency
Internation iliyotolewa hivi karibuni.
Ripoti hiyo mpya iliyotolewa Julai 11, mwaka
huu inaonesha kwamba kwa sasa Tanzania inaongoza katika nchi 35 za Afrika baada ya kupungua kwa vitendo vya rushwa
katika sekta nyingi, ambapo Ofisi ya Rais na Ofisi ya Waziri Mkuu zimeonekana
kuaminika zaidi.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwatahadharisha
watumishi wa umma kwamba Serikali kamwe haitomvumilia mtumishi atakayebainika anayejihusisha na vitendo vya rushwa na aliwataka
wahakikishe kuwa wanatekeleza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi bila ubaguzi.
Waziri Mkuu amesema Serikali imejipanga vizuri katika
mapambano dhidi ya rushwa, hivyo amewataka wananchi wasisite wakati wote kutoa
taarifa kwa vyombo husika pale watakapobaini uwepo wa watumishi wanaojihusisha
na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa.
“Watumishi wa umma wanatakiwa kutambua kwamba jukumu lao
kubwa ni kuwatumikia wananchi kwa kuzingatia maadili na kanuni za utumishi wa
umma zilizowekwa kwa mujibu wa sheria na kanuni na si vinginevyo. Serikali hii
kamwe haitowaonea haya au kuwafumbia macho watumishi wa hovyo.”
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema kuwa suala la kuwaondoa
kazini watumishi wazembe, wasiotimiza wajibu wao ipasavyo pamoja na wale
wasiozingatia maadili ya utumishi wa umma ni endelevu kwa sababu Serikali
inahitaji watumishi wa umma wenye heshima na nidhamu ya kazi.
Suala la kuwapokea, kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi
katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma kwa wananchi zikiwemo ofisi za
Serikali kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa ni miongoni mwa vipaumbele vya
Serikali ya Awamu ya Tano, hivyo watumishi wa umma wanapaswa kuzingatia jambo
hilo.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, JULAI 15, 2019
Post A Comment: