WANANCHI wa Kata ya Muhintiri iliyopo katika Jimbo la Uchaguzi la Singida Magharibi wamesema hawamtaki Mbunge mwingine katika jimbo hilo zaidi ya Elibariki Kingu.

Hatua hiyo imefikiwa na wananchi hao kufuatia maendeleo makubwa aliyoyafanya mbunge huyo kuanzia ujenzi wa shule, miradi ya maji, madaraja, Zahanati, miundombinu ya barabara, uimalishaji wa michezo pamoja na kujitoa kwake kusaidia jamii  kwa mambo mbalimbali.

Akizungumza wakati akimkaribisha mbunge huyo kuhutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata hiyo jana Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Muhintiri Maliko Deu alisema tangu wamepata Uhuru hakuna mbunge ambaye aliwahi kuwafikia wananchi kwa kuwapelekea maendeleo kwa kiasi hicho kama Kingu.

"Kwa kusema ukweli Kingu amegusa kila kitongoji cha jimbo letu katika kuleta maendeleo tunasema hatumtaki mbunge mwingine zaidi yake kwanza anamsaidia sana Rais wetu Dkt.John Magufuli na tunamuhakikishia katika uchaguzi mkuu ujao tutawapa kura za kutosha kuanzia  Rais, Mbunge na Diwani hao wapinzani walie tu" alisema Deu.

Akihutubia katika mkutano huo Kingu alisema katika kipindi cha miaka minne tangu wachaguliwe serikali ya awamu ya tano imefanya kazi kubwa ya maendeleo katika nchi hii baada ya Rais Dkt.John Magufuli kudhibiti fedha zilizokuwa zikitumika hovyo na kuziba mianya ya wizi na fedha hizo kuzielekeza katoka shughuli za maendeleo kama vile ununuzi wa ndege, ujenzi wa vituo vya afya, barabara, umeme, reli na miradi mingine.

Aliongeza kuwa mradi wa umeme unaojengwa mto Rufiji utaifanya nchi yetu kuwa ya tatu kwa uzalishaji wa umeme Afrika ambao tutauuza kwa nchi zingine na kuongeza pato la taifa.

Katika hatua nyingine Kingu alitoa maagizo kwa uongozi wa kata hiyo kuhakikisha wanaanza mara moja ujenzi wa wodi ya wajawazito ili kuwaondolea changamoto ya mahali pa kujifungua kwani fedha za kazi hiyo zilikwisha tolewa lakini wanao kwamisha ni Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kushindwa kuwapelekea ramani ndipo ujenzi uanze.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: