WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi, amesema serikali itaanza kusajili nyaraka na hati milki za ardhi ndani ya mkoa husika, badala ya utaratibu wa mwanzo  wa kusajiliwa ndani ya kanda zilizokuwa zimetengwa lengo ni kupunguza ucheleweshaji wa usajili wa nyaraka hizo na kuepusha usumbufu wa wananchi.


Waziri Lukuvi ametoa kauli hiyo leo Jijini Dodoma wakati akifungua, mkutano wa wataalamu wa sekta ya ardhi na wakurugenzi na makatibu tawala wa mikoa, wanaokutana jijini  Dodoma, kutathmini malengo ya sekta hiyo, sambamba na kuwajengea uwezo wataalamu  hao namna bora ya ufanyaji  kazi na namna ya kutatua changamoto zilizopo.

Amesema wamekusudia kuhamisha ofisi za kusajili nyaraka za ardhi kutoka katika kanda, na kuzirudisha ndani ya mikoa husika, ili kurahisisha zoezi hilo, na upatikanaji wa nyaraka hizo kwa wakati,  na tayari wakuu wa mikoa wameridhia na kutoa majengo yatakayotumika kama ofisi za wizara za usajili ndani  ya mikoa.

“Nataka hatimiliki zote zitolewe na kusajiliwa mikoani kwani watu wamekuwa wakipoteza muda na gharama nyingi za usafiriki kufuatilia hati hivyo hatuwatendei haki hawa wananchi wanyonge kwa kuwatwisha mzigo wa gharama”amesema Lukuvi.

Na katika kuhakikisha wananchi wanyonge wanapata huduma stahiki, amepiga marufuku wakuu wa idara za ardhi kupokea tozo ambazo hazistahili, pamoja na utumiaji wa madalali ndani ya ofisi za umma.

Amesema kuwa wananchi hivi sasa wamekuwa wakipatashida kupata hatimiliki zao za maeneo kutokana ofisi nyingi kuwepo katika maeneo ya kanda pekee yake.

Pia amesema yupo mbioni kuandaa kanzi data ya matapeli wa ardhi na kuiweka katika tuvuti ya wizara ya ardhi ili wananchi wawajue na kujiepusha nao ili wasitapeliwe ardhi zao na watu hao na hata muogopa mtu yeyote.


Waziri Lukuvi pia amesema kuwa haitakuwa na maana kwa serikali kama itaendelea kuwapa mzigo wa gharama wanachi wake wakati wa ufuatiliaji wa hati miliki za  maeneo yao na ndio maana wakaja na mpango huu.

“Tunataka kuwasaidia wananchi kupata hati miliki za maeneo yao huku gharama wanazozitumia ni nyingi leo hii unakuta mtu anatoka Kigoma anakuja Tabora, kufuata hati lakini tofauti na nauli anatumia siku saba hadi kumi kukamilisha zoezi hilo”, amesema

Mbali na hilo amewaonya watumishi wa idara za ardhi nchini kuacha tabia ya kupandisha bei ya maeneo pamoja na gharama za upimaji kwa madai kuwa wanajiongezea mapato ya ndani.

Amesema bei ya viwanja lazima ziwe kwamujibu wa sheria zilizowekwa na siyo kila mtu kujipangia bei zake ambazo zinageuka kuwa kero kwa wananchi na kubaki kumilikiwa na wachache wenye uwezo wa kifedha.

 Amemtaka katibu mkuu wa wizara hiyo Doroth Wanyika, kuhakikisha anapanga safu ya wakuu wa idara  haraka watakao kwenda kufanya kazi katika ofisi za wilaya na ofisi za mipango miji na orodha hiyo ipite mikononi mwake kabla ya wahusika kupewa barua za uteuzi.

Vilevile amesema wataanza kutumia tehama katika kurasimisha ardhi na wameanza katika mkoa wa Dar es saalam na unafanya  kazi kwa kasi sana na kuanzia mwakani zoezi hilo litakuwa la Tanzania nzima.

Amebainisha kuwa baada ya mkutano huo wataanza utaratibu wa kuwapisha kiapo cha maadili kwa watumishi wote kuanzia ngazi ya wizara hadi ngazi za chini ili kuhakikisha kila mtu katika kitengo  chake  anafanya kazi kwa uadilifu mkubwa kuleta mabadiliko chanya ndani ya wizara hiyo.

Katibu mkuu wa wizara ya Ardhi nyumba na maendeleo ya makazi, Doroth Mwanyika amesema kuwa lengo la kikao hicho ni kufahamiana na kuleta mapinduzi katika sekta ya ardhi nchini.

Amesema lengo jingine ni kupunguza migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikisababisha kudolola kwa shughuli za uzalishaji mali ikiwa ni pamoja na kuondoa tatizo la kiwanja kimoja kumilikishwa kwa mtu zaidi ya mmoja.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: