Na Mathew Kwembe-Chemba, Dodoma

Aliyewahi kuwa Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Chemba  iliyopo mkoani Dodoma Mwalimu David Mwamalasa ambaye hivi sasa amehamishiwa wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma amesimamishwa kazi na serikali kwa muda wa wiki mbili ili kupisha uchunguzi dhidi yake wa matumizi mabaya ya fedha kiasi cha shilingi milioni 259 ambazo zililetwa na serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ajili mradi wa P4R kwenye Shule za sekondari za Mondo na Soya  zilizopo wilayani Chemba, katika mkoa wa Dodoma.

Agizo la kumsimamisha Afisa Elimu huyo limetolewa jana na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Mwita Mwikwabe Waitara (MB) mara baada ya kufanyika mkutano wa hadhara shuleni hapo ambao uliwahusisha wanafunzi, walimu na wakazi wa kijiji cha Mondo, katika wilaya ya Chemba.

Sambamba na kusimamishwa kwa Afisa elimu huyo ambaye alihamishiwa wilayani Chamwino mkoani Dodoma, Mhe.Waitara amemwagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Joseph Nyamuhanga kuunda timu ya uchunguzi itakayokwenda shuleni hapo ili kuchunguza tuhuma hizo.

“Timu ije hapa ndani ya wiki mbili tupate fedha zilizoelekezwa kwa nini zimetumika kinyume na maelekezo, hayo ndiyo maelekezo yangu,” amesema Mhe.Waitara na kuongeza:

“Jambo lingine ambalo nimemwelekeza Katibu Mkuu, ni la kuhakikisha kuwa kuanzia sasa mtumishi anapofanya makosa eneo moja asihamishwe kwenda eneo linguine kwa nafasi yake ileile na kwa kweli hatupendelei kama viongozi, hata Mhe.Rais hataki, mtendaji yoyote ambaye atakuwa TAMISEMI amefanya makosa katika shule ya Mondo, natolea mfano kwa nafasi hiyo hiyo, hatuwezi tukawa tunasambaza uozo, kama mtu amekosa achukuliwe hatua, kama ni kuwa demoted (kushushwa cheo) ama kufukuzwa kazi ili na wengine wajifunze wasifanye makosa yale yale.”

Naibu Waziri amesema serikali haiwezi kuendelea kuwa na mtindo wa aina hiyo ambapo unafanya makosa sehemu A unahamishiwa sehemu B, badala yake akataka mhusika anapokutwa na makosa awajibishwe kwa kuondolewa nafasi yake ili apishe watumishi wengine ili wachukue nafasi hiyo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: