Wananchi katika Kijiji cha Chiboli wilayani Chamwino, Jimbo la Mtera, watasherehekea sikukuu ya Eid El-fitr wakiwa na umeme kwa mara ya kwanza, baada ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu kuwasha umeme katika Kijiji hicho.

Akiwa ameambatana Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, Naibu Waziri wa Nishati, amewasha umeme katika Zahanati ya Kijiji hicho pamoja na Kisima cha Maji ambapo Kijiji hicho kimepata umeme kupitia mradi wa BTIP (kV 400) ambao umesambaza umeme katika Vijiji 121 vinavyopitiwa na mradi kutoka Iringa hadi Shinyanga.

Akizungumza na Wananchi, Mgalu amesema kuwa, kuwashwa kwa umeme katika Kijiji hicho ni muendelezo wa utekelezaji wa adhma ya Serikali ya Awamu ya Tano kufikisha umeme katika Vijiji vyote nchini.

Amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani mwaka 2015 kulikuwa vijiji takribani 2,018 vyenye umeme na kuanzia Januari 2016, vijiji vipya vilivyoongezeka ni takribani 5000 hivyo hadi sasa vijiji 7290 vina umeme kati ya Vijiji 12,268.

Kuhusu usambazaji umeme katika maeneo ambayo hayajapata umeme ingawa yamepitiwa na miundombinu alisema kuwa, kuna mradi wa ujazilizi, mzunguko wa Pili unaolenga kuongeza wigo wa kuunganisha umeme katika vitongoji mbalimbali na Dodoma ni moja kati ya Mikoa 9 itakayoguswa na mradi huo.

Naibu Waziri, pia amesisitiza wananchi kutumia vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) ambavyo vitawawezesha kuondokana na gharama za wiring na kuwezesha kuunga wateja wengi katika mradi huo wa BTIP. 

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mtera, Lusinde alishukuru Serikali kwa kupeleka umeme katika Kijiji hicho, hata hivyo aliomba umeme huo ufike katika maeneo muhimu kama vile shamba la umwagiliaji, nyumba za ibada, na vitongoji vya Kijiji hicho.

Aidha, aliipongeza Serikali kwa kufanya kazi bila ubaguzi kwani idadi ya watu katika Kijiji hicho si kubwa ukiliganisha na vijiji vingine lakini Serikali haikungalia idadi ya watu ili kufikisha umeme katika Kijiji hicho wala hadhi ya nyumba.

Wilaya ya Chamwino, ina vijiji 107 na vijiji 54 tayari vimesambaziwa umeme huku kazi ya usambazaji  ikiendelea kupitia miradi mbalimbali kama REA Awamu ya Tatu  Mzunguko wa Kwanza na BTIP.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: