Monday, 10 June 2019

WAMILIKI WA MABASI YA ABIRIA NCHINI WAKUTANA NA MEYA TANGA.


Baadhi ya wamiliki wa mabasi ya abiria wakimsikiliza Meya wa jiji la Tanga (hayupo pichani).

Na Mashaka Mhando,Tanga

CHAMA Cha Wamiliki wa Mabasi ya Abiria (TABOA) na baadhi ya wasafiri Mkoani Tanga, wamekutana na Meya wa Jiji la Tanga, kuwasilisha kilio chao juu ya agizo, linalowataka ifikapo Juni 16 mwaka huu, vibanda vyote vya kukatisha tiketi za abiria kusafiri, vihamishiwe katika kituo kikuu cha mabasi kilichopo Kange Jijini Tanga.

Wakizungumza katika kikao hicho kilichoitishwa na TABOA na kufanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari Jumuiya, Wamiliki hao na abiria, walionesha wazi hawako tayari kuhamisha vibanda vya kukata tiketi za safari, wakieleza zitaleta usumbufu na kuongeza mzigo wa usafiri kwa wananchi.

Akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa TABOA mkoa wa Tanga, L’Abdi Awadh, alisema kikao hicho wamekiitisha na kukutana na Meya ili wawasilishe kilio chao cha kubatilishwa maamuzi hayo ambayo yalifanyika katika kikao kilichofanyika Mei 22 katika ofisi za Jiji la Tanga.

Kikao hicho kilichohudhuriwa na Mkurugenzi wa Jiji Daud Mayeji, Ofisa wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na majini (Sumatra) Dk Walukani Luhamba, Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Kamishina Mwandamizi Msaidizi (SACP) Eduward Bukombe, Kamanda wa usalama barabarani Solomon Mwangamilo na baadhi ya wasafirishaji ambapo wakatoa mapendekezo hayo ya kuondoka mjini.
 
“Mheshimiwa Meya kikao chetu tumekiitisha kwasababu ya kuomba pendekezo la kuondoa ‘Booking Office’ na kuzipeleka Kange kiukweli tutawaumiza wananchi tazameni upya, msigombane na wananchi, tunaomba mfikirie upya suala hili,” alisema Awadh ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Simba Mtoto.

Mjumbe wa Kamati ya Sumatra-CC Mariam Siafu alisema halmashauri ya Jiji itazame upya suala la ofisi za kukatishia tiketi kuhamia Kange kwani litamuumiza mno mwananchi hivyo ameiomba serikali kuingilia kati na kwavile serikali ni sikivu watasikilizwa na ofisi hizo zitaendelea kubaki mjini ili kuwarahishia wananchi ukataji huo.
 
Salimu El-Mazrui mkazi wa Jiji la Tanga, alisema kwamba suala hilo lisipotatuliwa vizuri na Meya huyo linaweza kumuanguisha katika uchaguzi ujao hivyo amemuomba asaidie kuokoa gharama zitakazokuwepo kwa wnanachi kwenda Kange kukata tiketi na kurudi kisha kwenda tena kusafiri.

Akizungumza katika mkutano huo Meya wa Jiji la Tanga, alisema kwamba ana waunga mkono katika suala la kudai ofisi hizo zibaki mjini lakini aliwapa angalizo kwamba lazima chama chao cha Taboa wawe na umoja usiyoyumba ili waweze kuwa na maamuzi ya pamoja kuliko sasa wamekuwa wakitofautiana.
 
“Kwanza nawapongeza kwa kuitisha mkutano huu ambao mimi nawaunga mkono kwa yote mnayozungumza, sioni kero isipokuwa mfuate taratibu katika kuwasilisha maepndekezo mapya maana inaonekana kikao cha tarehe 22 ni nyie ndiyo mliotaka kuhama Kange,” alisema na kuongeza kwamba wakutane wajumbe wao wachache waone ni jinsi gani watamaliza tatizo hilo

No comments:

Post a Comment