Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa  ameshangazwa na kitendo cha Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kugawa kiwanja kwa kikundi cha wajasiriamali cha Dulla Chunga kinachojishughulisha na uchongaji wa milango na madirisha ya chuma  katika eneo ambalo linajaa maji mengi kipindi cha mvua.

Dkt. Mary ameshangazwa na kitendo hicho mara baada ya kufika katika eneo hilo na kujionea changamoto alizoelezwa awali na wajasiriamali hao alipowatembelea katika eneo ambalo kwasasa wanafanya uzalishaji chini ya miti kutokana na ukosefu wa eneo rasmi.

“Nimeshangazwa sana na kitendo hiki kwani wajasiriamali hawa wamefuata taratibu zote za umiliki wa ardhi na wamekuwa wakilipa kodi ya ardhi kila mwaka tangu wamilikishwe kwenye eneo ambalo si salama kwakuwa linajaa maji nyakati za masika,” Mwanjelwa ameongeza.

Kufuatia hali hiyo, Dkt. Mwanjelwa ametaka ufafanuzi kutoka kwa Mkurugenzi wa Manisaa hiyo, John Mgalula ambaye hakuweza kutoa majibu stahili ya suala hilo kwa madai kwamba watumishi wote wa Kitengo cha Ardhi waliokuwa wakishughulika na suala hilo kuhamishiwa katika vituo vingine vya kazi.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo ameahidi kuwahamishia wajasiriamali hao katika eneo lililotelekezwa na mmiliki ajulikanae kwa jina la CHAVDA.

Kutokana na kutoridhishwa na majibu ya Mkurugenzi, Dkt. Mwanjelwa amemuagiza Mratibu wa MKURABITA, Dkt. Seraphia Mgembe ambaye ni msimamizi wa urasimishaji ardhi na biashara za wanyonge kufuatilia kwa karibu suala hilo na kumpa majibu kwa maandishi ili kubaini ukweli wa jambo hilo.

Hata hivyo, Dkt. Mwanjelwa amewapongeza MKURABITA na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa kushirikiana na kuweza kuvijengea uwezo vikundi vya wajasiriamali wadogo katika Manispaa na kuanzisha One Stop Centre ambayo imesadia kuharakisha taratibu za kurasimisha vikundi vya wajasiriamali wadogo katika Manispaa ya Morogoro hivyo kuongeza pato la taifa.

Dkt. Mwanjelwa amewataka kuweka mikakati zaidi ya kuwafikia wajasiriamali wengi zaidi ambao hawajarasimishwa ili waingizwe katika utaratibu huo ambao unawawezesha kupata elimu ya biashara pamoja na mitaji ili kukuza kipato chao.

“Jengeni utaratibu wa kufanya ufuatiliaji kwa wajasiriamali ambao tayari wamesharasimishwa ili kujua changamoto wanazokutana nazo na kwa wale ambao hawajarasimishwa muwatafute ili waweze kunufaika na mpango wa Serikali wa urasimishaji,” Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.

Kwa upande wake Mratibu wa MKURABITA, Dkt. Seraphia Mgembe amemshukuru Naibu Waziri kwa kufanya ziara ya kutembelea vikundi vya wajasiriamali na kujionea hatua zilizofikiwa na taasisi yake katika utoaji huduma ya kurasimisha biashara za wanyonge kwa kuwa imewaongezea mbinu zaidi katika utekelezaji wa majukumu yao ambapo ameahidi kutekeleza maelekezo yote ya Naibu Waziri.

Katika ziara yake, Dkt. Mwanjelwa ametembelea vikundi vya usindikaji wa vyakula na viungo, Mafundi seremala, Mafundi wa makochi na maturubai ya magari pamoja na watengenezaji wa milango na madirisha ya chuma.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: