Friday, 14 June 2019

WAFANYABIASHARA SEKTA YA MADINI WAIPONGEZA BAJETI.

Mkurugenzi wa Tanzanite One Faisal Juma.

Na Mashaka Mhando, Arusha.

CHAMA cha Wanunuzi  na Wauzaji wa Madini nchini (TAMIDA) na wachimbaji wadogo wa madini ya vito mkoa wa Arusha na Manyara, wameipongeza bajeti ya serikali ya mwaka 2019/20 kwa kuondoa kodi za mashine za kukata madini.
Mwenyekiti wa TAMIDA, Sammy Mollel amesema bajeti ya mwaka 2019/20 imeondoa kilio cha muda mrefu cha wachimbaji  na wauzaji wa madini nchini.
Mollel alisema kuondolewa kwa kodi za mashine za kukata na kusanifu madini, kutaongeza ajira kwa vijana wengi lakini kutaongeza mapato ya serikalini kwani madini mengi yatasanifiwa na kuongezwa ubora hapa nchini.
Mkurugenzi wa kampuni ya Tanzanite One na Tanzanite Forever Faisal Juma alisema uamuzi wa serikali kuondoa  kodi katika mashine za kukata madini ni faraja kwa sekta ya madini.
“kuondoa kodi katika mashine za kukata madini, inamaana watanzania wengi wataanzisha viwanda vidogo vya kusanifu madini”alisema.
Alisema viwanda hivyo, licha ya kukata madini na kusanifu na kuondoa changamoto zilizokuwepo, pia kutawasaidia vijana wengi kupata ajira ya moja kwa moja.
"Kwa kitendo hiki walichofanya serikali kuondoa kodi, wametuongezea ufanisi kwa kiwango cha juu lakini pia vijana wetu watapata ajira," alisema Juma ambaye ana mashine 30 za kuchakata madini na ameajiri vijana wakutosha.
Juma pia alipongeza bajeti kwa kuanzisha dawati la kusikiliza malalamiko ya wafanyabiashara wanapokuwa na malalamiko ya kodi kwani sasa kutaongeza uwazi na uwajibikaji.
Alisema kulikuwa na shida TRA hasa suala la malalamiko ya makadirio ya ulipaji wa kodi hivyo kuwepo kwa chombo hicho kutaondoa ukiritimba na usumbufu wa ulipaji kodi za makadirio.
“kulikuwa na shida unakadiliwa kodi hakuna sehemu ya kulalamika lakini pia hata TRA walikuwa hawawezi kushusha bila kupata muafaka sasa kutakuwa na chombo cha tatu ambacho kitamaliza migogoro”alisema.
Mkurugenzi huyo alimpongeza Rais kwa kuonesha kwamba amekuwa na nia madhubuti ya kuwasaidia wafanyabiashara kwa kuondoa mlolongo wa kodi zaidi ya 54 ambazo zilikuwa zikimnyonga mfanyabiashara nchini.
"Tunamshukuru Rais nia yake ni kila mfanyabiashara anakuwa bora na hii namnukuu kauli yake aliyotuambia pale Ikulu, anataka akiondoka aache mabilionea Watanzania," alisema na kuongeza kwamba watamuunga mkono asilimia 100.

No comments:

Post a Comment