Friday, 14 June 2019

UN Migration yatoa vifaa Tiba Hospitali Murugwanza na Nyamiaga


Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo (Mb) amepokea vifaa tiba vyenye thamani ya Sh milioni 142 kwa ajili ya Hospitali teule ya Murugwanza na hospitali ya Nyamiaga wilayani Ngara vilivyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wahamaji (IOM).

Katika makabidhiano ya vifaa tiba yaliyofanyika kwenye Ofisi za Wizara jijini Dodoma Waziri Jafo ameiagiza kurugenzi ya afya kuangalia namna ya kununua vifaa vya kisasa kama vilivyokabidhiwa na IMO kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma 352 ikiwamo kifaa ya upasuaji ambacho kinazuia utokwaji wa damu.

Jafo pamoja na kulishukuru Shirika la IOM, aliitaka kurugenzi ya afya kuangalia namna ya kuwa na vifaa vya kisasa katika vituo vya kutolea huduma 352 vinavyoendelea kujengwa Nchini.

“Hii mashine ni ya kisasa, ambayo daktari anaweza kufanya upasuaji hata kwa mama mjamzito mwenye damu kidogo kwasababu inauwezo wa kuzuia utokwaji wa damu wakatiwa upasuaji.

“ Wote tunajua kuwa suala la damu kwa mama wajawazito ni tatizo, na hata upatikanaji wa damu kwa wakati ni shida huku usalama wa damu yenye kwa sasa ni wa mashaka.

“Sasa tukiwa na kifaa kama hiki badala ya daktari kuhangaika kutafuta kumuongezea damu mama mjamzito ili amfanye upasuaji kwa kuwa na kifaa hiki anaweza kufanya upasuaji hata mwenye damu 5.

Jafo aliongeza: “ kwa sasa tunaenda kukamilisha vituo vya kutolea huduma za afya 352 na tumeanza kujenga hospitali za wilaya 67 na hospitali mpya 27 zitaanza kujengwa katika mwaka ujao wa fedha, basi niagize kurugenzi ya afya tukiwa tunaenda kwenye hatua ya kununua vifaa tuangalie aina hii ya vifaa.

Alisema mashine hiyo ya kufanyia upasuaji inauzwa kati ya Sh milioni 3 hadi nne wakati kifaa ambacho kinaweza kumsaidia daktari kupata mwanga wakati wa upasuaji hata kama hakuna nishati kinauzwa kati ya Sh laki 6 na laki 6.

Awali, Mwakilishi Mkazi wa IOM, Dk Qasim Sufi alisema taasisi yake iko katika mikoa 11 ya Tanzania na ikiwa na wafanyakazi 200 na 180 kati ya hao ni watanzania.

Alisema shirika hilo limekuwa likishughulikia kuwalinda wa hamaji ikiwa ni pamoja na kuwarejesha nyumbani wakimbizi.

“Unaweza kujiuliza imekuwaje IOM kusaidia vifaa vya kutolea huduma kwa hospitali hizi? Hii imetokana na tukio ambalo lilimetokea tukiwa kwenye operesheni ya kuwarejesha nyumbani wakimbizi wa Burundi.

“Kulitokea ajali ambayo ilisababisha vifo vya watu 8, na majeruhi wengi waliweza kuokolewa kwa kupatia matibabu kwenye vituo hivi viwili, lakini kulikuwa na chagamoto ya vifaa kwani mimi mwenye niliingia kusaidia katika kuokoa maisha ya watu.

Dk Sufi aliongeza: “ni tukio ambalo bado nalikumbuka, na sisi IOM bado tunaendelea na majukumu yetu na lolote linaweza kutokea huko, hivyo tukaoana tusaidie hospitali hizi mimbili vifaa mbalimbali ikiwamo hiki cha upasuaji ambacho kinaweza kumfanya mgonjwa asivuje damu nyingi, kwani tuliowapoteza walikuwa wamevuja damu nyingi.

No comments:

Post a Comment