Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imetangaza mikakati mipya ya kuhakikisha inaendelea kupata watalii zaidi toka nchini China huku ikibainisha pia kuwa imejipanga kutangaza mazao ya misitu nchini humo ikiwemo asali.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya TTB Jaji Mstaafu Thomas Mihayo alisema kwamba viongozi kutoka nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki wamepanga kufanya ziara nchini China kwa ajili ya kuimarisha utangazaji wa vivutio vya utalii katika nchi hiyo ya Asia ya Mashariki.

Jaji Mihayo alisema kuwa kiongozi wa msafara huo utakao ambatana maafisa mbalimbali kutoka TTB na wizara ya Utalii na Maliasili atakuwa ni Naibu Katibu Mkuu wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Aloyce Nzuki.

Alieleza kuwa ziara hiyo ya wiki moja nchini China itaanza Juni 19 hadi 26 mwaka huu katika miji minne. Miji itakayotembelewa na ujumbe huo kutoka Tanzania kwa mujibu wa Jaji Mihayo ni Beijing, Shanghai, Nanjing na Shangsha, lengo pia likiwa ni kuhakikisha Tanzania inaongeza sehemu ya umiliki wa soko la utalii China.

Jaji Mihayo aliongeza kuwa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) na vyanzo vingine vya habari habari duniani vimebainisha kuwa soko la utalii la China linaendelea kuongoza kuwa na idadi kubwa zaidi ya watalii na mchango mkubwa katika uchumi wa dunia.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: