Saturday, 22 June 2019

Shule ya Mfano Dodoma haiendani na viwango vya Mfano

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.
Selemani Jafo(Katikati) akiwasilia katika eneo la ujenzi wa shule ya mfano katika
Mkoa wa Dodoma inayojengwa katika kata ya Ipagala
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.
Selemani Jafo akitoa maelekezo wakati wa ziara yake kukagua maendeleo ya
shule ya mfano ya Mkoa wa Dodoma inayojengwa katika Kata ya Ipagala Jijini
Dodoma.

 
Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani
Jafo(Mb) amesema ujenzi unaoendelea wa shule ya mfano inayojengwa Mkoani
Dodoma haiendani na viwango vya mfano ambavyo mtu yeyote akija atatambua kuwa
hiyo ndio shule ya mfano.


Akikagua maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo ya Msingi inayojengwa katika Kata ya
Ipagala Jijini Dodoma wakati wa ziara yake Waziri Jafo ameyasema alitegemea kukuta
kitu kitofauti na alichokikuta eneo la ujenzi kwa sababu Dodoma ndio Makao Makuu ya
Nchi.
“Ujue mpaka shule inapewa hadhi ya kuwa ya mfano inatakiwa iwe ya utofauti mkubwa
sana na shule za kawaida kuanzia kwenye ramani ya majengo, ukubwa wa eneo,
muonekano wa majengo yanayojengwa, mandhari, viwanja vya michezo na kila kitu
kitakachowekwa katika shule hiyo” Amesema Jafo


Aliongeza kuwa Sasa kwa hapa Ipagala kwanza ukiingia tu unaanza kuona eneo la
shule limezingirwa na makazi ya watu kwa karibu sana halafu majengo yanayojengwa
yote ni ya chini kama mabehewa ya Treni hamuoni kwa eneo lililopo hapa hamtapata
nafasi ya kutosha kwa ajili ya kufanya vitu vingine vya Msingi.


Aidha Mhe. Jafo alifafanua kuwa “eneo mlilonalo la Ekari saba sio dogo kwa ujenzi wa
shule ya kawaida lakini sio lakini kubwa kwa ujenzi wa shule ya mfano yaan hapa
mlitakiwe mpate ekari hata thelathini kuwe na nafasi ya kutosha kisha mjenge majengo
ya gorofa, vipatikane viwanja vya michezo vizuri, maeneo ya kupumzikia watoto na
nyumba za walimu ziwe pembeni kidogo sio vitu vyote visongamane katika eneo moja;
Hii ni shule ya mfano inatakiwa kuwa na muonekano ambao kila mtu akija hapa
atakubali kuwa kweli hapa ni eneo la mfano na wengine watakuja kujifunza kwaiyo
sitafurahia kuona vitu vya kawaida kawaida tu lazima mjue kujiongeza”.


Aliongeza kuwa sitegemei kuona shule hii inafanana na shule ya Msingi Chaduru au
Nzuguni B lazima iwe tofauti katika kila kitu, mkifanya mchezo nyie Dodoma ndio
mtakuwa tofauti na wenzenu wote wanaojenga shule hizi za Mfano na watawazidi
endeleni kufikiria kawaida tu.


Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Belnith Mahenge alikiri
kuwa wataalamu wa Dodoma hawakupanua mawazo yao katika kuangalia namna bora
ya kutekeleza ujenzi wa shule ya mfano katika Mkoa wa Dodoma.

“Nikiri tu kuwa tumekosea na baada ya ziara hii ya Mhe. Waziri tukaa pamoja na
wataalamu wetu kuangalia namna gani tunaweza kurekebisha kasoro hizi zilizojitokeza
katika ujenzi huu wa Shule ya Mfano ili iwe na ubora unatakiwa katika shule hizi”
Alisema Mahenge.


Naye Mkurgenzi wa Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI Julius Nestory ametaja vigezo vya
shule za Mfano kuwa ni Uwepo wa Vyumba vya madarasa kuanzia 17 tofauti na shule
za kawaida ambazo zina vyumba sita mpaka tisa na shule hiyo itajengwa eneo lenye
idadi kubwa ya watu ambapo pia kutakua na idadi kubwa ya wanafunzi.


Nestory aliendelea kutaja vigezo vya shule ya mfano kuwa ni uwepo wa miundombinu
muhimu kama Nyumba za Walimu, Maktaba, Ukumbi wa Mikutano, Jengo la Utawala,
vyoo vya kutosha pamoja na viwanja vya michezo.


Alimaliza kutaja maeneo ambayo shule hizo zitajengwa Nchini kuwa ni Dodoma eneo la
Ipagala, Kigome kule Buhigwe, Geita, Mtwara katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi
na Mara kwenye shule aliyosoma Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere ambayo ni Shule
ya Msingi Mwisenge.


Naye Afisa Elimu Msingi Jiji la Dodoma Joseph Mabeyo amesema walipokea Tsh Mil
706 mnamo mwezi April 2019 na ujenzi unaondelea utahusisha vyumba vya madarasa
17, Maktaba, Bwalo la chakula, nyumba za walimu, matundu ya vyoo pamoja na Jjengo
la Utawala na ujenzi huo unategemea kukamilika Mwezi Agosti, 2019.


No comments:

Post a Comment