Serikali imesema hadi Desemba 31, mwaka huu, Watanzania wote wenye sifa za kupata vitambulisho vya Taifa watakamilisha usajili wa kuchukua alama za vidole, picha na saini ya kielektroniki, kazi inayoendelea kufanywa sasa.

Sambamba na hilo, serikali imesema itanunua mashine mpya za uzalishaji wa vitambulisho vya taifa zenye uwezo mkubwa zaidi kwa lengo la kuharakisha upatikanaji vitambulisho hivyo.

Hayo yalibainishwa bungeni na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni wakati akijibu swali la mbunge wa Buyuni, Christopher Chiza (CCM). Mbunge huyo alihoji serikali ina mpango gani wa kuharakisha zoezi la kutoa vitambulisho vya taifa wavitumie kwa shughuli za maendeleo.

Akijibu swali hilo, Masauni alisema serikali kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), inaendelea kukamilisha usajili kwa watu wote wenye sifa ikitarajiwa kukamilisha kazi ya uchukuaji alama za vidole, picha na saini ya kielektroniki Desemba 31, mwaka huu.

Alisema hadi sasa vitambulisho milioni tano vya taifa vimeshatolewa na kwamba vingine milioni 13 vipo hatua za mwisho kutolewa na kwamba hadi ifikapo Desemba mwaka huu, lengo lao ni kutoa jumla ya vitambulisho milioni 24.4. Wananchi waendelee kuwa watulivu na wale waliokamilisha uchukuaji alama za vidole, saini na picha na hawajapata vitambulisho, huenda ndio hivyo milioni 13 vilivyo hatua za mwisho kutolewa,"alisema Naibu Waziri Masauni.

Aidha alisema katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bila kukwama ikiwemo wale wanaojisajili kibiashara Brela, NIDA imefungua dawati maalum la usajili katika ofisi hizo. Alisema usajili huo unafanywa kwa kuzingatia sifa bila kuathiri masharti ya kisheria na kanuni.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: