Na EZEKIEL NASHON,
DODOMA.
SERIKALI Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Seleman
Jafo, amewataka wakurugenzi kote nchini kuhakikisha wanasimamia
kikamilifu miradi inayotekelezwa katika halmashauri zao ili iweze
kuleta matokeo chanya.
Ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo
ya wakurugenzi yaliyoandaliwa na chuo cha serikali za mitaa Hombolo
yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kuandika maandiko ya miradi ya kimkakati
katika halmashauri zao.
Amesema lazima wakurugenzi wahakikishe wanasimamia kikamilifu
miradi hiyo kwani nia ya serikali kutekeleza miradi hiyo ni kuhakikisha miradi
hiyo inawanufaisha wananchi katika maeneo husika ni lazima isimamiwe na
kutekelezwa kwa viwango.
“Serikali inawekeza fedha nyingi sana katika miradi hii ni
wajibu wenu sasa kuhakikisha mnaisimamia kikamilifu lengo la serikali
kuhakikisha wananchi wananufaika na miradi hii, simamieni kikamilifu” amesema.
Aidha amesikitishwa na kitendo cha baadhi ya mikoa
kama Dodoma na Njombe kushindwa kufika katika kikao hicho na baadhi
ya mikoa kama Mtwara,Lindi kuleta wakurugenzi wachache ukilinganisha na
halmashauri zilizopo katika mikoa hiyo.
Amesema mafunzo hayo yanaumuhimu mkubwa kwa wakurugenzi
kuwajengea uwezo wa kuwawezesha katika kuandika maandiko ya kimkakati lakini
wanapuuzia mafunzo hayo.
“kuna wakurugenzi siwaoni hapa kama wa Dodoma au kwavile
wanakusanya mapato kuliko wengine na kujiona? Ukiangalia mkoa wa Dodoma kuna
mradi mmoja tu kule Kondoa, hii mingine ni ya serikali kuu,
ukiangalia Njombe hawana mradi hata mmoja lakini hawapo” amesema.
Ameagiza kuandaliwa kwa kikao kingine ndani ya mwezi mmoja
na kuwaagiza wawezeshaji wa kikao hicho kuwapa taarifa
wakurugenzi mapema ili waweze kuhudhuria kikaohicho kwani kinaumuhimu
sana kwa wakurugenzi na kuagiza kila halmashauri kuhudhuria.
Pia amewataka wawezeshaji wa kikao hicho kujenga utaratibu wa
kuwatembeza wajumbe wa vikao hivyo katika miradi inayotekelezwa ili
waweze kujifunza na wao wakatekeleze katika maeneo yao.
Kwa upande wake kaimu mkuu wa chuo cha serikali za mitaa
Hombolo, Michael Msendekwa amesema lengo la kuandaa kikao hicho ni kuwajengea
utaratibu na uwezo wa kuandika maandiko ya miradi kwani kwa utafiti wao
waligundua kuna shida katika uandishi wa miradi.
“Tumeandaa mafunzo haya kwa sababu kwa utafiti tuliofanya
tumegundua kunashida katika uandishi wa maandiko kwa wakurugenzi
wetu tukaona ni mda mwafaka kwa kuwajengea uwezo” amesema.
Post A Comment: