Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi akizungumza wakati alipokutana na wasimamizi wa huduma za Afya katika jiji la Dar es Salaam (RHMT) kujadiliana mbinu mbali mbali ili kuweza kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, hususan katika kipindi hichi cha milipuko ya magonjwa ya Dengue na Kipindupindu.

Na WAMJW- DSM
Serikali imeagiza Waganga Wakuu wote kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji wa kila kifo kitakachotokea katika Hospitali zote nchini ili kubaini chanzo cha vifo hivo jambo litalosaidia kuimarisha mikakati katika kupambana na magonjwa, hususan magonjwa ya milipuko.

hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi leo wakati alipokutana na wasimamizi wa huduma za Afya katika jiji la Dar es Salaam (RHMT) kujadiliana mbinu mbali mbali ili kuweza kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, hususan katika kipindi hichi cha milipuko ya magonjwa ya Dengue na Kipindupindu.

Dkt. Subi amesema kuwa katika vita dhidi ya magonjwa ya mlipuko ni lazima kushirikiana na taasisi nyingine kama vile DAWASA ili kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa kurekebisha na kuimarisha miundombinu ya maji ambayo yanaweza kuwa moja ya chanzo cha mlipuko wa magonjwa hayo.

Pia, Dkt Subi amesema kuwa moja ya makubaliano ya kikao hicho ni kuhakikisha inapofika Juni 30, ugonjwa wa Dengue uwe umekwisha katika jiji la Dar es Salaam.

"Wamenihakikishia kwamba inapofika tarehe 30, wamesema mbinu zote inatumika kuhakikisha ugonjwa wa homa ya Dengue unaisha jijini Dar es Salaam au unapungua kwa kiwango ambacho hautoonekana" alisema Dkt Leonard Subi.

Aidha, Dkt Subi amemwagiza Mganga Mkuu kuhakikisha wanatumia taarifa zote za wagonjwa ambao wanafariki kutoka na magonjwa ya Kipindupindu pamoja na ugonjwa wa homa ya Dengue ili kupata takwimu sahihi ya vifo vinavyosababishwa na magonjwa hayo.

Aliendelea kusema kuwa Serikali imefanikiwa kupambana dhidi ya ugonjwa wa Kipindupindu, huku ikifanikiwa kupunguza maambukizi ya homa ya Dengue kutoka wagonjwa 1000 kwa mpaka kufikia wagonjwa 200 kwa wiki, na jitihada zinaendelea kuchukuliwa ili kuutokomeza kabisa ugonjwa huu.

Mbali na hayo Dkt. Subi alisisitiza kuwa katika mapambano dhidi ya mbu anaesababisha homa ya ugonjwa wa Dengue ni lazima kushirikisha wananchi katika ngazi ya Jamii ili kutoa elimu ya kutosha juu ya namna yakuzuia ugonjwa huu.

Kwa upande mwingine, Dkt. Subi amemwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha anashirikiana na Wakurugenzi ili kutimiza ahadi za kununua mashine za kunyunyizia maazalia ya mbu ambao wanasababisha ugonjwa wa Dengue.

Hata hivyo, Dkt Subi ameagiza watu wote wanaobainika kutapisha maji machafu katika mazingira kuchukuliwa hatua kali kupitia sheria ya Afya ya jamii ya mwaka 2009.

Nae Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Yudas Ndungile amemshukuru Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt Leonard Subi kwa muda aliotenga ili kufahamu kiundani hali ya utendaji kazi katika Sekta ya Afya katika ngazi ya mkoa na ameahidi kutekeleza maagizo yote ili kuendelea kuimarisha Sekta ya Afya.

Mwisho.
Share To:

Post A Comment: